Polisi Arusha Wasambaratisha Utafiti wa Nani Mkali kati ya LOWASSA na MAGUFULI Uliokuwa Ukifanywa Mitaani!

Wakati tafiti za kienyeji zenye lengo la kupima kukubalika kwa wagombea urais, hasa Dk John Magufuli na Edward Lowassa zikizidi kuongezeka, polisi jijini Arusha mwishoni mwa wiki walitumia nguvu kutawanya vijana waliokuwa wakiendesha kura za maoni kwenye stendi ndogo ya mabasi na soko kuu.

Tangu kutangazwa kwa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi za Twaweza na Ipsos, vijana kwenye maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko, hasa sokoni na kwenye baa wamekuwa wakiendesha tafiti zao za kienyeji wakiwa na lengo la kuonyesha hali halisi ilivyo mitaani tofauti na matokeo ya tafiti hizo mbili.

Katika tafiti hizo za Ipsos na Twaweza, Dk Magufuli, ambaye anagombea urais kwa tiketi ya CCM, alikuwa mbele ya Lowassa anayegombea kwa tiketi ya Chadema na vyama vinavyounga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini matokeo hayo yamepingwa vikali na wadau mbalimbali, huku yakiamsha tafiti za kienyeji mitaani.
Katika tukio lililotokea mjini Arusha, vijana walikuwa wakiendesha utafiti wao kwenye soko kuu la Arusha na eneo la kituo kidogo cha mabasi, lakini polisi walifika na kuwatimua wakidai wanavunja sheria.

Wafanyabiashara hao wa soko hilo na stendi ndogo, waliandaa maboksi mawili ya kura, moja likiwa limeandikwa “Magufuli” na jingine “Lowassa”. Baadaye walialika watu kwenda kupiga kura.

Kila aliyepita katika eneo hilo alielezwa utaratibu wa kupiga kura na alitumbukiza karatasi yake katika boksi lililoandikwa jina la mgombea anayeona anafaa kuwa rais.

Utafiti wa stendi ndogo ulikamilika baada ya muda na ulionyesha matokeo ya wagombea hao (tunayo).

Wakati watu waliokuwa stendi ndogo wakiendelea kushangilia matokeo hayo, wafanyabiashara wenzao wa soko kuu walikuwa wakiendelea kupiga kura na ghafla polisi walifika maeneo hayo na kuwatimua vijana waliokuwa wakikusanya kura.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema waliokuwa wanafanya utafiti huo walikiuka sheria na kwamba kitendo chao kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuwa kulikuwa na watu wasioafikiana.

Aliwataka wakazi wa Arusha kuacha kufanya mambo ambayo hayana manufaa, badala yake wasubiri siku ya kupiga kura.
“Huo ni utafiti wa aina gani wa maboksi?” alihoji alipoulizwa kuhusu tukio hilo.
“Hizi ni vurugu za mitaani. Tunawaomba wananchi watulie, wasubiri siku ya uchaguzi wapige kura kwa amani.”

Hili ni tukio la pili la utafiti unaofanywa kienyeji mitaani baada ya wafanyabiashara wa Kariakoo, Dar es Salaam kuendesha utafiti wao kwa kuruhusu watu kumpigia kura mgombea wanayempenda kati ya Magufuli na Lowassa.

Mbali na utafiti huo wa wakazi wa Dar es Salaam, kwenye maeneo mengine nchini kumekuwapo na watu wanaoendesha tafiti kama hizo zenye lengo la kujua ni mgombea gani wa urais anakubalika zaidi.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini