Msafara wa mgombea urais wazuiliwa

Msafara wa mgombea urais kupitia chama cha ACT­ Wazalendo umezuiwa kwa muda na wananchi wa Wilaya ya Nachingwea, wakidai kuwa na wao wanahitaji baraka kutoka kwa mgombea huyo baada ya kuzikosa kwa muda mrefu. 


Kitendo cha kusimamishwa katika eneo la soko la Nachingwea Mjini, kilimlazimu mgombea Anna Mghwira, kuwahutubia akiwa barabarani huku akilakiwa na umati mkubwa wa watu. 


Kama vile haitoshi wananchi hao walimlazimisha mgombea huyo kwenda kwenye kiwanja cha Nachingwea, ili kuwaeleza ni kwavipi chama chake kitapambana kuondoa umasikini unaowakabili. 


“Nashuka tuandamane hadi huko kiwanjani wapiga kura wangu” alisema mgombea huyo na kuandamana na wananchi hao kuelekea kwenye viwanja vilivyoko karibu na soko la Nachingwea. 


Ilimchukua muda wa saa moja mgombea huyo kueleza sera za chama chake kwa wananchi wa Nachingwea na kuahidi kuzifanyia kazi kero mbalimbali mara watakapompa ridhaa ya kuongoza Tanzania. 


Mghwira alianza kwa kuelezea vipaumbele vya ACT Wazalendo endapo kitaingia madarakani. 


Alivitaja vipaumbele hivyo ni pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii, ambapo aliwaahidi wananchi hao kuingizwa katika mfumo utakaowawezesha kujiwekea akiba na hivyo kuwasaidia katika matibabu na hata maisha ya baadaye. 


“Katika utawala wangu kila mmoja atafaidika na mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii. Sitakuwa tayari kusikia Mtanzania anashindwa kujihudumia wakati wa ugonjwa au wakati akiwa amezeeka na hafanyi kazi tena,” alisema.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini