SUMAYE Ampa Makavu MAGUFULI...LOWASSA Aahidi Kudhibiti Rushwa Ndani ya Siku 100

Jana ilikuwa ni Septemba 26 ambapo UKAWA waliendelea na mikutano yao ya kampeni za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi .Jana ilikuwa ni zamu ya wakazi wa Wilaya ya Hai ambapo Waziri Mkuu wa zamani, Fredrik Sumaye aliendelea na kazi ya kupangua mashambulizi ya CCM.

Sumaye aliitumia siku ya jana kumjibu Dk Magufuli aliyesema kuwa utafiti uliofanywa na Twaweza unaoonyesha anaongoza kwa asilimia 65, umempunja ushindi aliostahili.

Sumaye alisema Dk Magufuli hawezi kupata hata asilimia 40 ya kura na ndiyo maana amekuwa akitofautiana na mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete.

Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni uliofanyika Rundugai, Jimbo la Hai, Sumaye alisema Dk Magufuli amekuwa akikisahau hata chama chake na kuwataka wananchi wachague Tanzania ya Magufuli, huku akiomba wananchi wasichome godoro lote lenye kunguni badala yake waue kunguni waliopo kwenye godoro hilo.

“Haiwezekani mkalalia kitanda chenye kunguni si ndiyo,” alihoji Sumaye na kuitikiwa na wananchi “ndiyoooooo”.
“Amesahau hata kusema chagua CCM, anasema chagua Tanzania ya Magufuli,” alisema Sumaye na kuongeza kuwa Tanzania haiwezi kuwa ya Magufuli, bali ni ya Watanzania wote.

Sumaye alisema kuwa hali ya CCM ni mbaya na ndiyo maana wananchi wamechoka na hali zao ni mbaya.
“Wananchi wanataka mabadiliko, hakuna vita itakayotokea kama wanavyohubiri huo ni upuuzi mtupu,” alisema Sumaye.
Sumaye aliwaambia wananchi hao wa Rundugai kuwa nchi nyingi duniani zinapata mabadiliko kwa kubadilisha mfumo uliopo, hivyo wananchi wasiogope kwa kuwa CCM siyo mama yao, bali ni chama cha siasa.

Lowassa Aahidi Kudhibiti Rushwa Ndani Ya Siku 100
Wakati Sumaye akisema hayo ,mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa aliahidi kuhakikisha anapambana na tatizo la rushwa ambalo limekuwa chanzo cha umasikini nchini.

"Siku 100 za serikali ya Chadema, tutaunda chombo kila wilaya ambacho kitakuwa ‘one stop centre’. Ukienda mjini kwa shughuli za kiserikali huduma zote zitakuwa sehemu moja, hii itaondoa urasimu na rushwa." Alisema Lowassa.

Huku akionekana kujiamini kushinda katika chaguzi ujayo,Lowasa alisema atahakikisha anaongoza nchi kwa misingi ya haki na usawa huku akiahidi kutumia vema ilani ya ukawa kuhakikisha anapambana na rushwa.

Alisema kwa mara ya kwanza nchini Tanzania upinzani utachukua nchi na akasisitiza kuwa CCM lazima Ing'oke mwaka huu.
"CCM lazima ing'atuke mwaka huu, lakini itang'atuka kwa kura zenu, hivyo nawaombeni mtunze sana vichinjio vyenu." Alisema Lowassa na kuongeza;

“Wale wenzangu waliochukia mimi kuondoka CCM, sasa wameanza kukubali uamuzi wangu kwa kuwa CCM imeshindwa kuongoza nchi, haifai tena kuongoza kama Sumaye alivyosema.Hali ya wananchi ni mbaya sana."

Lowassa aliendelea kurudia ahadi zake za elimu bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu, pia kuboresha maisha ya Watanzania waondokane na umaskini ambao kila siku amekuwa akisema anauchukia.

Katika mkutano huo, Lowassa alimsihi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuendelea kuambatana naye kwenye kampeni ili aongeze nguvu kwenye timu yake.

Lowassa alisema Mbowe anaweza kufanya kampeni zake kwenye Jimbo la Hai na kuweka timu ambayo itamsaidia wakati atakapokuwa nje ya jimbo kumpigia kampeni mgombea urais.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbowe aliiponda CCM akisema kwa sasa haijielewi kwa kuwa iko hoi.

Alisema katika uchaguzi huu hawatakubali kuibiwa kura huku akiwaomba askari wakae pembeni ya siasa na kulinda amani ili wanasiasa wacheze ngoma yao wenyewe.
“Askari wetu lindeni amani tuachieni CCM tucheze nao msipendelee upande wowote,” alisema Mbowe.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini