UKAWA Mnajiangusha Wenyewe -MAKAMBA
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba.
Na Elvan StambuliMjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba (pichani) amesema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unajiangusha wenyewe katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu kutokana na wanayoyafanya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Makamba alisema migogoro ndani ya Ukawa katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi imesababisha mitafaruku katika kuachiana majimbo na hata wakati wa uteuzi wa mgombea urais, hivyo umoja huo utakosa ushindi.
Makamba alisema migogoro hiyo imesababisha viongozi wa muda mrefu na maarufu wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa CUF na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa kujiondoa katika chama hivyo kupunguza imani ya wananchi kuhusu uwezo wa vyama hivyo kushika dola.
Aliongeza kwamba kazi kubwa anayofanya mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli na mgombea wake mwenza, Samia Suluhu Hassan ya kuzunguka nchi nzima kwa barabara na kuongea moja kwa moja na wapiga kura vijijini imezaa matunda kwani wananchi wanaonesha kuwaunga mkono kwa kuwa wanawaelewa tofauti na wapinzani wao wanaotumia ndege.
Makamba alisema hata wagombea ubunge na udiwani wa CCM na makada na viongozi wa chama katika ngazi zote nchi nzima kila siku wanafanya kazi za ziada za kumuombea kura mgombea wao, jambo ambalo alisema limezaa matunda ya ushindi.