Iringa walalamikia wagombea kuwaomba kura vilabuni wakinywa pombe
Wananchi wa vijiji vya Mufindi Kaskazini wamelalamikia baadhi ya wagombea wa vyama vya siasa kufanya kampeni zao za kuomba kura kwenye vilabu vya pombe za kienyeji.
Vijiji vya Mufindi Kaskazini ni ukelemi, Uyele, Saadani, Mbugi, Tambalangíombe, Uhambila, Lugoda, Mapogolo pamoja na Ikweha.
Akizungumza na waandishi wa habari mmoja wa wakazi wa kitongoji cha Ulaya kijiji cha Ikwea, Lutego Blastus, alisema toka zimeanza kampeni hawajawahi kuwaona wagombea wa vyama vya siasa kufanya kampeni zao, lakini kuna mgombea mmoja wa udiwani kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), alikwenda kufanya kampeni kwenye klabu cha pombe.
Sisi wanakijiji tunaomba wawe wanakuja kufanya kampeni zao kwenye sehemu zenye viwanja maana mtu akifanya kampeni kwenye kilabu anakuwa kama anatudanganya maana wakati huo tunakuwa tumelewa,î alisema.
Naye, Elimas Waya, alisema wanawaomba wagombea waende kufanya kampeni kwenye kijiji chao kwani tangu zilipoanza wamemuona mgombea huyo mmoja tu ambaye alienda kufanya kampeni kwenye klabu.
Pia wanakijiji hicho walisema pamoja kutowaona wagombea wa vyama vingine kufanya mikutano kwenye kijiji chao bado wataendelea kumuenzi Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuhakikisha wanachagua viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Waya alisema kuwa bado hajaona matatizo ya CCM ndio maana katika kijiji chao hawapendi kusikia vyama vingine huku akiwataka wanasiasa hao waache kupotosha watu wakiwa wamelewa na kwamba kama wanataka kufanya kampeni ni vyema wakafuata utaratibu waliopangiwa.