MWENDESHA BODABODA ACHINJWA KAMA KUKU NA MTU ALIYEKODI PIKIPIKI

Kijana mmoja mwendesha pikipiki maarufu kama bodaboda aitwaye Ismail Khalid(25)mkazi wa mtaa wa Shilabela kata ya Kalangalala mjini Geita ambaye ni mwenyeji wa Nyakahula wilaya ya Biharamlo mkoani Kagera ameuawa kikatili kwa kunyongwa kisha kuchinjwa akitenganishwa kichwa na kiwiliwili na mtu aliyekodi usafiri wake wa pikipiki.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Desemba 19  mwaka huu saa 5 usiku baada ya mtu ambaye hakufahamika mara moja kufika eneo la Stand mpya anapopaki pikipiki yake na kumkodi akimtaka ampeleke katika mtaa wa Tambukaleli mjini Geita.

Inaelezwa kuwa mtu huyo alimnyonga na kumchinja shingo kwa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili chake na baadaye kutokomea kizani na pikipiki hiyo.
Kaka wa marehemu Hassan aliiambia blog hii  kuwa,mwili wa mdogo wake uligundulika asubuhi ya Desemba 19 mwaka huu mita chache kutoka eneo alilokuwa akipaki pikipiki yake.

Kwa mujibu wa majirani kwenye eneo la tukio inavyoonekana wauaji walimuulia eneo hilo na kutokomea na pikipiki hiyo ambayo hata hivyo namba zake hazikuwezaa kupatikana mara moja.
Mwenyekiti wa bodaboda wilaya ya Geita Daniel Dotto mbali na kuthibitisha kuwepo kwa mauaji hayo amelitupia lawama jeshi la polisi ambapo amedai kuwa mbali na matukio ya bodaboda kujeruhiwa,kuuawa na hata kuporwa pikipiki,kutikisa mji wa Geita wanapowakamata watuhumiwa hao baadaye huachiwa na kuwatambia mitaani.
Alisema jeshi la polisi ndilo linachangia kuendelea kwa matukio hayo kwa kuzembea kuwachukulia hatua watuhumiwa.

"Siyo leo tu ,haya matukio ni ya kila siku lakini cha ajabu tunapowakamata watuhumiwa,hususani wanaoiba pikipiki zikiwa zimepakiwa na wengine kujifanya madeiwaka, tunapowafikisha polisi wanaachiwa baada ya siku mbili,hii inakatisha tamaa sana’’aling’aka Dotto mbele ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wilaya ya Geita.
Kwa upande wake mkuu huyo wa upelelezi wa makosa ya jinai wilaya ya Geita,John Maro akizungumza na bodaboda hao katika mkutano wa dharula kujadili suala hilo ameahidi kuwapatia ushirikiano na kutishia kuwawajibisha askari wote watakaobainika kuwakingia kifua wahalifu wa utekaji wa waendesha bodaboda.

Na Valence Robert

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini