Hii Hapa SIRI YA MAFANIKIO Kutoka Kwa CHEUSI wa SIRI YA MTUNGI!

Katika tamaduni za kimagharibi mtoto ana uhuru wa kuchagua afanye nini au ajikite kwenye taaluma gani ambayo anaona inafaa au kumvutia.
Wazazi nao huwa mstari wa mbele kumsaidia mtoto kwa kumuewekea mazingira rafiki ili aweze kutimiza azma au ndoto yake.

Tofauti na ilivyo katika tamaduni za Kiafrika ambapo wazazi ndiyo hutoa muongozo wa kile wanachotaka watoto wao wafanye katika maisha.

Inapotokea mtoto au kijana akachagua kufanya kitu tofauti na matakwa ya wazazi wake huonekana mkaidi na anayejitafutia kuwa na maisha mabaya.

Pamoja na kuwapo kwa kasumba hiyo wapo watoto ambao wanasimamia kile wanachokiamini na kukiweza hivyo kujikuta wakifanikiwa na kuwashangaza wazazi.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mwigizaji Godliver Gordian nyota wa tamthilia ya ‘Siri ya Mtungi’ anayefahamika zaidi kama Cheusi.

Wengi walimfahamu Cheusi kupitia tamthilia hii iliyovuta hisia za watazamaji wa vipindi vya runinga alipocheza kama mke wa mhusika mkuu Cheche.

Pamoja na kuwa na uwezo mkubwa katika uigizaji Cheusi ni mwanahabari taaluma ambayo aliipata kinyume na matakwa ya baba yake ambaye alitaka awe askari.
“Baba yangu alikuwa askari na hakuna mtoto wake wa kiume hata mmoja ambaye alifuata nyayo hizo, hivyo akawa anataka binti yake nimrithi kazi hiyo.

“Ilinibidi kumtia moyo lakini nilipomaliza sekondari na kutaka kujiunga na Chuo nililazimika kumwambia ukweli kwamba napenda kuwa mtangazaji hivyo nataka kusomea uandishi wa habari.”

Anasema alifanikiwa kumshawishi baba yake baada ya kumuahidi kuwa ataenda jeshini baada ya kumaliza elimu yake ya chuo itakayomuwezesha kupata vyeo ndani ya muda mfupi.

Alijiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari na kupata cheti cha stashahada huku dhamira yake ikiwa ni kutangaza redioni.

Akiwa katika harakati za kutafuta kazi aliamua kujiingiza kwenye uigizaji fani ambayo alikuwa akiipenda tangu utotoni ndipo alipofanikiwa kukutana na Single Mtambalike aliyemchezesha kwenye filamu ya Mahabuba.
“Nilicheza katika filamu chache lakini ikatokea ghafla siitwi tena sikujua sababu ilikuwa nini nikaamua kuendelea na mambo mengine ingawa moyoni mwangu niliamini kuwa naweza sanaa.

Ilipita muda kidogo ndipo nilipopewa taarifa na rafiki yangu kuhusu usahili ya waigizaji wanaotakiwa kucheza ‘Siri ya Mtungi’ nami nikajitosa kwa vile niliamini naweza na hivyo ndivyo ilivyokuwa nilifanikiwa kupata nafasi hiyo.

Ilifika wakati ilibidi wazazi wangu wakubaliane na ninachokifanya na kuniunga mkono hali iliyozidi kunipa faraja na morali ya kusonga mbele zaidi.”

Anabainisha kuwa ujasiri na msimamo wake umechangia kwa kiasi kikubwa kumfikisha alipo leo licha ya kupitia vikwazo mbalimbali ikiwemo kukatishwa tamaa lakini aliongeza juhudi na kusonga mbele.

Uwezo mkubwa alioonyesha Cheusi ambaye kwa sasa yupo chini ya usimamizi wa kampuni ya Saseni Media ulimuwezesha kupata nafasi ya kushiriki kwenye tamthilia na filamu kadhaa ikiwemo Home Coming inayotarajiwa kutoka hivi karibuni.

Wanawake na uchaguzi 
Cheusi anawapa changamoto wanawake hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi kuwa makini wakati wa kufanya uamuzi ili kuwachagua viongozi wenye sifa na nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo.
“Katika kipindi cha uchaguzi mengi yanatokea na wanawake ndiyo tunakuwa wahanga wakubwa huku tukitumika kama daraja kuwapitisha watu wenye wanaotaka kukidhi matakwa yao.

Tusikubali zawadi za kanga, fedha au kujazwa chuki na maneno ya jazba tuwe na muda wa kusikiliza sera na kuchuja zuri na baya kabla ya kufikia uamuzi wa kumchagua mtu,” anasema.

Nyota huyu ambaye ni mama wa mtoto mmoja anasema hakuna kitu anachokitamani kiendelee kuwepo nchini kama amani na utulivu.

Anasisitiza kuwa wanawake wana nafasi kubwa ya kuhakikisha amani inaendelea kuwepo na kujenga misingi ya upendo na utulivu kuanzia kwenye ngazi ya familia mpaka taifa kwa ujumla.
“Tanzania inasifika ulimwenguni kote kama kitovu cha amani tuna kila sababu ya kuiendeleza sifa hiyo, tuache hasira na chuki bali upendo utawale hasa kwenye kipindi hiki cha uchaguzi”
Chanzo: Gazeti la Mwananchi

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini