ANGALIA PICHA MATESO ANAYOPATA DADA
Kaseli James mwenye umri wa miaka 29, mkazi wa Kijiji cha Stela Kata
ya Kagea Wilaya ya Chato, mkoani Geita, anapata maumivu makali mwilini
mwake kufuatia uvimbe mkubwa katika mdomo wake, unaomsumbua kwa muda wa
miaka minne sasa.
Bi. Kaseli James, akiwa na uvimbe mkubwa mdomo wake . Licha ya
kupata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa kipindi chote
hicho, lakini maumivu yake yamekuwa yakiongezeka kila siku huku
wataalamu wa hapo wakishindwa kutambua tatizo hasa linalomsumbua.
Akisimulia mkasa uliompata, wakati huu akiwa amelazwa katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili, Kaseli anasema alijisikia vibaya baada ya kuambiwa
hivyo, kwani hakuwa na fedha na wala hakujua ni nani angeweza
kumsaidia.
“Nilikata tamaa nilipoambiwa na madaktari kwamba matibabu yangu mpaka
Muhimbili, niliamini ningefia kijijni kwetu, lakini Mungu alinipa nguvu
nikawa napita kwa ndugu na maskini wenzangu walinichangia hadi zikafika
shilingi 50,000 nilifanya nauli, wakati nakuja hata hela ya kula njiani
sikuwa nayo, nilifika na kulazwa,” alisema.
Tatizo lake lilianza mwaka 2010 alipojisikia kupata uchungu wa jino,
uliofuatiwa na kuota kwa kijipele ambacho baadaye kilitumbuka kama vile
ni jipu.
“Kimsingi tangu nianze kuumwa sijawahi kupata matibabu ipasavyo,
tatizo sina hela, hata kule nyumbani mara nyingi nilijiuguza kienyeji
tu, huku mdomo ukiendelea kuvimba na kushindwa kula vizuri,” alisema
mama huyo.
Aliongeza kuwa, wakati akiwa bado mzima, alijaaliwa kupata mtoto na
mwanaume aliyemtaja kwa jina la Frank Samson, lakini baada ya ujauzito
baba huyo aliingia mitini na kumtelekeza bila huduma yoyote hadi hivi
sasa.
Mwanamke huyo ambaye amelazwa Wodi namba 24 Jengo la Sewa Haji,
anasema amefanyiwa vipimo, lakini bado tatizo lake kubwa litakuwa ni
gharama za matibabu, kwani hata kaka yake aliyeongozana naye hana sehemu
ya kulala wala kula.
Muonekano wa karibu wa uvimbe huo. “Nimekuja na kaka ili aweze
kufuatilia matibabu yangu lakini ndiyo hatuna uwezo wa kipesa na wala
mahali pa kulala kaka yangu, kwa kweli tupo katika wakati mgumu
sana.“Huko nyumbani kwetu hatuna ndugu mwenye uwezo ambaye anaweza
kutusaidia wala hatuna vitu vya thamani ambavyo tungeviuza na kupata
fedha za kugharamia matibabu yangu.
“Kwa kifupi maisha yetu ni magumu kwani kule kijijini tunategemea
kilimo cha jembe la mkono, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kuna
wakati tunakosa mavuno hivyo kuwa na tatizo la chakula.
“Nitoe shukrani kwa madaktari na manesi wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili, walionipokea vizuri na hadi muda huu nimeshapimwa vipimo
mbalimbali nasubiri majibu, lakini ndiyo bado kilio changu kipo kwenye
gaharama za matibabu,” alisema Kaseli.
Mama huyo anasema kuwa baada ya kuondoka wilayani Chato kwenda
Muhimbili kimatibabu, mwanaye aliyemtaja kwa jina la Modesta Frank,
alimuacha kwa baba yake mzazi (babu) ambaye ni mzee akiwa na hali mbaya
kiuchumi hivyo haelewi wanaishije.
Kwa yeyote aliyeguswa na matatizo ya mama huyu, anaweza kuwasiliana
naye kwa namba yake ya mkononi 0754 912453 au kumtembelea Wodi Namba 24,
Jengo la Sewa Haji Hospitali ya Taifa Muhimbili.