WATOTO WADAIWA KUMUUA BABA YAO KWA KUMPIGA FIMBO WAKIMTUHUMU KUUZA CHAKULA CHA FAMILIA
JESHI la Polisi mkoani Kagera linawashikilia watoto watatu, kwa tuhuma za kumpiga fimbo kichwani baba yao mzazi na kumsababishia kifo.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Gilles Muroto, alisema tukio hilo ni la mwezi Septemba 15, mwaka huu katika Kijiji cha Mkunyu Kata ya Kikukuru Tarafa ya Mabira wilayani Kyerwa.
Alisema
siku ya tukio, watuhumiwa hao, ambao hakuwataja majina yao kutokana na
umri wao kuwa chini ya miaka 18, walimuua baba yao, Henry Siliakus (62)
kwa kumchapa fimbo kichwani akiwa nyumbani kwake hadi akapoteza uhai
wake.
Muroto alisema watoto hao, mmoja wao ana umri wa miaka 17, anasoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Mkunyu.
Mwingine
ana umri wa miaka 13, anasoma darasa la nne. Mwingine ana umri wa miaka
11, anasoma darasa la tatu. Wote wawili wanasoma katika Shule ya Msingi
Mkunyu.
Kamanda
alisema sababu ya awali ya mtafaruku huo, uliosababisha kifo ni ugomvi
wa baba na watoto wake, kwa kile kinachodaiwa baba yao kuwa na tabia ya
kuuza chakula cha familia na kuwaacha wakitaabika na njaa.
Kamanda
alisema jeshi hilo, bado linaendelea na uchunguzi wa kina juu ya tukio
hilo na litawafikisha mahakamani watoto hao pale taratibu za kisheria
zitakapokamilika.