HABARI KAMILI KUHUSU MAANDAMANO YA CHADEMA NA KIBANO CHA POLISI
Mtikisiko mkubwa wa kisiasa jana umelikumba taifa, baada ya wafuasi wa Chadema kupambana na polisi katika maeneo mbalimbali.
Hali hiyo, ilianza kuonekana mapema jijini Dar es Salaam, wakati
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwapowasili Makao Makuu ya Jeshi
la Polisi saa tano asubuhi kwa ajili ya kuhojiwa.
Mbowe aliitwa kuhojiwa na viongozi wa jeshi hilo kwa madai ya kutoa kauli za uchochezi wiki iliyopita.
Akizungumza kwenye mkutano wa Kamati Kuu ya chama chake, Mbowe
alisema wataitisha maandamano na migomo isiyokuwa na kikomo nchi nzima
kuishinikiza Serikali kusitisha Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea
mjini Dodoma.
Mbowe aliwasili polisi saa 5 asubuhi akisindikizwa na msafara wa
magari matano yaliyobeba baadhi ya wanachama, mawakili na viongozi wa
chama hicho.
Baada ya kuwasili katika eneo hilo, wanachama hao walipinga kiongozi
wao kushuka ndani ya gari hadi atakapoingia ndani ya lango kuu.
Wanachama hao walisikika wakisema ‘Peoples’ huku wengine wakiitikia ‘Power’.
Kitendo hicho kilipingwa na polisi waliokuwa wakilinda lango hilo na
kuamuru Mbowe ashuke na kuingia kwa miguu ndani ya jengo hilo.
Kitendo hicho kilionekana kuwakera wafuasi waliokuwa wamekusanyika
eneo hilo na kuamua kusukuma lango hilo kwa nguvu ili waweze kuingia
pamoja na kiongozi wao.
Kutokana na hali hiyo, wafuasi hao waligoma na kuanza kupambana na
polisi ambao nao walijihami kwa kuzuia geti la lango wakiwa ndani.
Baada ya mabishano ya muda mrefu, ndipo polisi walipokubali Mbowe
aingie na gari ndani ya jengo hilo huku wakizuia msafara wa magari
mengine.
Kutokana na uamuzi huo, mawakili walilazimika kushuka ndani ya gari.
Mmoja wa askari aliyekuwa getini hapo, alisikika akisema anayepaswa kuingia ndani ya jengo ni Mbowe na mawakili wake.
“Tumekubaliana gari linaloingia ndani ni moja tu la mwenyekiti, msilazimishe matumizi ya nguvu,” alisikika akisema askari huyo.
Kitendo hicho kilipingwa na wanachama hao huku wakitaka wabunge, mawakili na viongozi wengine waingie ndani.
Kutokana na hali hiyo, polisi walikubali na kuwaruhusu viongozi hao
kuingia ndani huku wakiwaamuru wanachama wengine na waandishi wa habari
kusimama umbali wa mita 200 kutoka kwenye lango hilo.
Baada ya kutokea kwa tangazo hilo, wafuasi hao walikaidi amri hiyo na
kusababisha askari D. D. Zahoro kuamuru kutumika nguvu kuwatawanya
pamoja na waandishi wa habari hali iliyosababisha kujitokeza kwa vurugu
katika eneo hilo.
Vurugu hizo zilidumu kwa muda wa saa moja na kusimamisha shughuli
mbalimbali zinazoendelea ndani ya jengo hilo na njia kufungwa kwa muda.
Katika vurugu hizo,wafuasi wanne wa chama hicho walikamatwa.
MWANDISHI APIGWA
Katika tukio hilo, mwandishi wa habari wa Gazeti la Tanzania Daima,
Josephat Isango alijikuta akishambuliwa vibaya na askari kwa virungu.
Licha ya Isango kuonyesha kitambulisho, polisi hawakutaka kumsikiliza
zaidi ya kuendelea kumshushia kipigo na kumsababishia maumivu katika
mguu wa kulia.
Kipigo hicho kilisitishwa baada ya waandishi wengine kupiga kelele
kuwaomba polisi kumwachia kwa sababu alikuwa kwenye majukumu yake ya
kazi.
MBOWE AHOJIWA
Wakati tukio hilo likiendelea, Mbowe alikuwa ndani ya jengo hilo akiendelea kuhojiwa akiwa na mawakili wake sita.
Mawakili hao, ni Peter Kibatala, Profesa Abdallah Safari, Mabere Marando, Nickson Tugala, Tundu Lissu na John Malya.
Mahojiano hayo yalianza saa tano na kudumu kwa zaidi ya saa nne.
Ilipofika saa 8:49 mchana, mawakili wanne wakiongozwa na Lissu walitoka
nje na kuzungumza na wafuasi na waandishi wa habari.
“Mwenyekiti yuko salama, aliitwa kwa ajili ya mahojiano na yamefanyika vizuri chini ya mawakili.
“Polisi wameomba tuzungumze na nyie tuwaombe muondoke kwa sababu
mwenyekiti akitoka na mkiwa wengi kunaweza kukawa na uvunjifu wa amani,”
alisema Lissu.
Baadhi ya wanachama hao walisikika wakisema hawawezi kuondoka kwa sababu hawawaamini polisi.
“Sisemi nawaamini polisi au la, tumekubaliana kwamba mwenyekiti
atapata dhamana, hivyo haitakuwa busara tukiondoka kwa maandamano,
tulikuja kwa amani hatutaki mtu atoke hapa akiwa amedhurika,” alisema
Lissu.
Baadhi ya wafuasi walikubali kuondoka huku wengine wakibaki.
Saa 9:17 alasiri, Mbowe alitolewa kwa kupitia mlango wa nyuma wa
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, huku akisindikizwa na magari manne
kwenda Kituo cha Polisi Kati ambako aliachiwa kwa dhamana.
MTIKILA
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher
Mtikila alifika eneo hilo akiwa kwenye bajaj, lakini alizuiwa kuingia
ndani.
DODOMA
Polisi mjini Dodoma, jana waliimarisha ulinzi kwa ajili ya kupambana
na wafuasi wa Chadema waliopanga kuandamana kupinga Bunge Maalumu la
Katiba linaloendelea mjini humo.
Miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na ulinzi mkali ni pamoja na jengo la
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Viwanja vya Nyerere Square na
mitaa mbalimbali ya mjini hapo.
Polisi waliweka uzio wa kamba kilipo Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE)
na makutano ya barabara jirani na stendi ya mabasi ya abiria
yanayokwenda mikoani ili kutoruhusu watu na magari kuelekea eneo la
Bunge.
Jengo la Bunge lilikuwa limezungukwa na askari wengi wenye silaha,
farasi na mbwa kuhakikisha usalama unakuwapo katika eneo hilo.
Ndani ya eneo la Bunge, nako ulinzi ulikuwa mkali kwani kulikuwa na idadi kubwa ya askari waliokuwa na silaha pamoja na mbwa.
Viwanja vya Nyerere
Katika viwanja vya Nyerere ambako wakazi wa Dodoma hupenda
kukusanyika kwa ajili ya kupumzika na kupata huduma za chakula na
vinywaji, jana shughuli zilisimama kwa muda kwa kuwa polisi walikuwa
wameweka ulinzi tangu asubuhi.
Nje ya viwanja hivyo, kulikuwa na vijana waliokuwa na mabango
likiwamo lililosomeka ‘Sitta tumia busara ahirisha Bunge la Katiba’.
Katika viwanja hivyo, polisi walionekana wakiwa wamekamata vijana wapatao kumi waliodaiwa kuwa walikuwa wakitaka kuandamana.
Wakati hali ikiwa hivyo katika maeneo hayo, ulinzi pia uliimarishwa
katika mitaa mbalimbali ya mji huo kwani askari polisi waliokuwa na
silaha na askari kanzu, walikuwa wametanda kila kona.
Chini ya ulinzi huo, magari yaliyokuwa yamejaa askari polisi yakiwamo
ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), yalikuwa yakizunguka
kila kona kuhakikisha hakuna maandamano yatakayofanyika.
Gari la Chadema
Pamoja na askari kuimarisha ulinzi huo, gari la Chadema lenye namba
za usajili T 792 CAX likiwa na nembo ya M4C, nalo lilikuwa likipita
katika mitaa ya mji huo ingawa haikufahamika lilikuwa likifanya hivyo
kwa maana gani.
Kuanzia saa 12 alfajiri jana, ofisi za Chadema Mkoa wa Dodoma
zilizoko eneo la Mji Mpya, zilikuwa zikilindwa na askari polisi
waliokuwa na silaha.
Radio za kijamii zafungwa
Katika hali ambayo haikujulikana wazi, radio za kijamii za mjini hapa
hazikuwa hewani jana asubuhi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kudhibiti
mawasiliano kati ya Chadema na wananchi.
Taarifa zilizopatikana baada ya mawasiliano hayo kukatika, zinasema
redio hizo hazikuwa hewani kwa saa kadhaa jana kwa vile viongozi wa
Chadema walikuwa wakizitumia kuhamasisha wananchi.
Miongoni mwa waliodaiwa kutumia redio hizo ni Mwenyekiti wa Chadema
Mkoa wa Dodoma, Jella Mambo ambaye awali alihamasisha maandamano hayo
kupitia Redio Kifimbo na Nyemo FM.
Hata hivyo, taarifa nyingine zinasema redio hizo hazikuwa hewani kwa
kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) walikuwa wakifanya
marekebisho ya masafa.
Akizungumza na mwandishi jana, Mambo alikiri kutumia redio hizo kuhamasisha maandamano kwa kuwa yalikuwa halali.
Pamoja na hayo, alisema kama Jeshi la Polisi limedhamiria kudhibiti
maandamano yao, linatakiwa kuandaa fedha nyingi ili kukabiliana nayo.
“Hapa Dodoma maandamano yapo ila tunayafanya kimkakati kwani watu
wametawanyika maeneo mbalimbali kila mmoja ana mabango yenye ujumbe
tofauti, yakiwamo tunayompongeza Rais Jakaya Kikwete kwa busara yake
aliyoitumia kutaka mchakato wa Katiba Mpya usikamilike kabla ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015,” alisema Mambo.
Wakati huo huo, Mambo alisema gari moja la Chadema lililokuwa
limebeba wajumbe wa Mkutano Mkuu waliokuwa wakitoka Dar es Salaam
kuelekea Mwanza, lilikamatwa na askari polisi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Emannuel Lukura alikiri kukamatwa kwa gari na wafuasi wanne wa chama hicho.
MBEYA
Habari kutoka mkoani Mbeya, zinasema polisi wameendelea kutunushiana
misuli na Chadema kuhusu kufanyika au kutofanyika kwa maandamano ya
kupinga kuendelea kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Chadema imesisitiza kufanyika kwa maandamano hayo leo. Mratibu Kanda
za Nyanda za Juu Kusini, Franky Mwaisumbe jana alisema kuwa
licha ya polisi kudai kuwa maandamano hayo ni batili, wao watahakikisha
yanafanyika kwani lengo lao ni kufikisha ujumbe kwa wananchi.
Alisema wao wanachokifanya ni kutimiza azimio la Kamati Kuu lililotolewa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema hadi jana jioni maandamano hayo yalikuwa hayajaombewa kibali.
ARUSHA
Mkoani Arusha, Chadema kimethibitisha kufanya maandamano leo, huku
kikisema tayari majimbo 14 kati ya 33 yamewasilisha barua katika vituo
vya polisi kwa ajili ya taarifa.
Katibu wa Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa akizungumza
kwa njia ya simu jana, alisema tayari wamekwishajipanga kuhakikisha
wanafanya maandamano ya amani ambayo hayatasababisha usufumbufu kwa watu
wala kuvunja sheria yoyote.
“Lengo letu ni ujumbe ufike kwa wabunge Dodoma, kwamba kikao
wanachoendelea nacho hakitatupa Katiba mpya. Sasa maandamano haya
tumeyapa kwa mfumo wa pekee kabisa,” alisema.
Habari hii imeandaliwa na Patricia Kimelemeta, Nora Damian na Shabani
Matutu (Dar es Salaam), Maregesi Paul, Rachel Mrisho na Debora Sanja
(Dodoma), Pendo Fundisha (Mbeya) na Elia Mboneya (Arusha) wa Gazeti la Mtanzania