Wauza unga watumia utashi kukwepa mkono wa Dola kuuza dawa za kulevya
TATIZO
la kuwepo na dawa za kulevya nchini bado ni kubwa na ukubwa uliopo
imebainika kuwa haulingani na kiwango cha juhudi za kudhibiti tatizo
hilo miongoni mwa wanajamii huku wauzaji wakiendelea kutumia mbinu
mbadala kwa lengo la kufanikisha biashara hiyo.
FikraPevu imefahamishwa
kuwa licha ya Jeshi la Polisi kupiga vita dawa hizo kwa kushirikiana na
vyombo vingine vya dola pamoja na viongozi wa madhehebu ya dini
biashara hiyo bado inaendelea kushamiri katika maeneo mbalimbali nchini
hususani mikoa ya Dar es Salaam na Kanda ya Kaskazini wakitaka kupata
utajiri wa haraka.
Wakiongea kwa nyakati tofauti na FikraPevu baadhi
ya wananchi wa jiji la Tanga wamesema kuwa, matumizi ya dawa za kulevya
kwa sasa ni tatizo sugu nchini ukiwemo mkoa huo na kwamba kwa sasa hali
hiyo imekuwa kwa kasi kutokana na magari yanayofanya safari katika
mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kutumiwa kusafirisha dawa hizo bila
kukamatwa na Polisi.
Walipoulizwa
kwanini wanafikiri biashara hiyo imeshamiri zaidi katika maeneo mengi
nchini, wamesema biashara hiyo inakuwa kutokana na kuhusisha watu wenye
fedha nyingi na miongoni mwao ni viongozi wa juu serikalini na hivyo
zoezi la kukomesha biashara hiyo haliwezi kufanikiwa.
Wakazi
wa jiji la Dar es Salaam wameeleza kuwa pamoja na kuwepo kwa Tume ya
Kudhibiti Dawa za Kulevya biashara hiyo inaendelea kufanyika bila
wahusika kukamatwa baada ya wengi wao kuhusishwa na biashara hiyo.
Mmoja
wa wakazi hao, Andrew Hamza (25) mkazi wa Manzese na mwendesha Bajaji
jijini humo ameitaka serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya dawa za
kulevya na kuanzisha Mahakama maalumu ya kushughulikia wahalifu wa dawa
hizo ili kuendana na majira kwani nguvu inayotumika kudhibiti wahalifu
hao hailingani na kile kinachotendeka na kwamba vijana ndio
wanaoathirika zaidi.
“Vijana
tunaoendesha Bajaji tunakutana na vitu vingi, unaweza kumwambia mteja
kumpeleka mahali flani kiasi kikubwa cha hela lakini hajali anaitoa tena
wakati ukimsikiliza akiongea na simu unajua kabisa kwamba hapa kuna
dili la dawa za kulevya, tena anakupa mashariti makubwa kweli kwahiyo
serikali ikawabana wanaoagiza itasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na
hili tatizo” aliieleza FikraPevu.
Baadhi
ya wakazi wa Kijitonyama wanasema zipo mbinu mpya za kutambua sehemu
inayouzwa dawa hizo “Ukipita majira ya saa mbili hadi saa tano asubuhi
katika mitaa hii (Karibu na barabara ya Afrika sana-Mabatini) ukiona
akina mama wamekaa tu bila kazi au vijana alafu wamechoka choka alfu
uone mfuko meusi umening’inizwa juu au raba jua hapo ndio penyewe,
lazima wawe na mzigo wa bangi au gomba (mirungi)”.
Amesema
ni wakati mwafaka kwa Bunge na serikali kuona uzito wa tatizo la dawa
za kulevya kutokana na ukweli kwamba katika miaka ya karibuni tatizo
hilo limeongezeka kwa kasi kubwa hali inayosababisha athari kubwa za
kiuchumi.
Ripoti
mpya ya hivi karibuni ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na
Mihadarati na Uhalifu imetamka wazi kwamba Tanzania ni kinara wa
kupitisha dawa hizo katika nchi za Afrika Mashariki, na mkoa wa Tanga
ulitanjwa kuwa ndio kiini cha mpaka unaotumiwa na wahalifu kusafirisha
madawa hayo.
Tangu
mwaka 2006, Rais Kikwete, alipotangaza vita dhidi ya wauzaji dawa za
kulevya kumewahi kuripotiwa mzozo miongoni mwa viongozi wa dini, baada
ya Rais Kikwete kueleza kuwa, baadhi yao wanahusika na biashara hiyo.
Kauli
yake iliwafanya viongozi wakuu wa dini nchini kumtaka awataje viongozi
hao lakini kwa upande mwingine, baadhi ya wafanyabiashara wa dawa hizo
walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere,
wakienda nchi jirani wakiwa wamezihifadhi katika sehemu za siri ili
zisikamatwe huku takribani vijana 300 wakiripotiwa kutumikia kifungo
katika mataifa ya China na Brazili kwa tuhuma za kukutwa na dawa hizo.
Viwanja vya Ndege
Jeshi la Polisi (kitengo cha) Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) mara kwa mara limekaririwa naFikraPevu likithibitisha
kukamata raia mbalimbali wa kigeni kutoka mataifa ya nje wakiwa na
gramu nyingi za dawa kulevya aina ya cocaine, Mirungi, na Bangi huku
wengi wao wakiendelea kutesa mitaani na katika mataifa yao bila
wasiwasi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini, Kamanda, Godfrey Nzowa, anasema juhudi za kupamba na kundi hilo bado
zinaendelea ambapo amekiri kuwepo kwa mbinu nyingine mpya zinazotumiwa
na wahalifu kusafirisha na kuuza dawa hizo nchini na kwamba wanazijua.
“Hapa
nchini hakuna sehemu inayotengenezwa madawa haya lakini uchunguzi
unaonyesha kuwa yanatoka nje Cocein na dawa nyingine tukiachilia mbali
mirungi na bangi ambayo inatapikana katika baadhi ya maeneo nchini”.
Kumekuwepo na kilio cha muda mrefu kuhusu tatizo hilo ikiwemo
taarifa zinazotolewa na raia wema kuhusu wafanyabiashara hao ambao hadi
leo asilimia kubwa ya watu hao wanaendelea kujineemesha kupitia
biashara hiyo.