MTOTO ALIYEMBAKA MTOTO MWENZIYE NA KUMPA MIMBA AHUKUMIWA KUCHAPWA VIBOKO 20


MKAZI wa Kijiji cha Karundi, Wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa, Moses Kang'ombe (17), amehukumiwa adhabu ya kuchapwa viboko 20 baada ya kupatikana na hatia ya ubakaji na kusababisha mimba.
 
Hukumu hiyo imetolewa juzi na Mahakama ya Wilaya hiyo baada ya kumtia hatiani katika makosa mawili la ubakaji na kusababisha mbakwaji ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba (jina tunalihifadhi), kupata mimba na kushindwa kufanya mtihani wa kuhitimu mwaka huu.
 
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ramadhani Rugemalila, alisema mshtakiwa alikiri kosa hivyo Mahakama ilimtia hatiani chini ya kifungu cha 130 (1) na (2)( e) na 131 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2002.
 
Alisema katika kosa la kubaka, atachapwa viboko 12 na kosa la kumpa mimba mwanafunzi huyo, atachapwa viboko vinane.
 
Awali Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Hamimu Gwelo, aliiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo mwaka huu na baada ya mwanafunzi huyo kukutwa na mimba.
 
Aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa mshtakiwa iwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kuwabaka wanafunzi na kuwasababishia mimba.
 Mahakama ilitoa adhabu hiyo kwa kuzingatia umri wa mshtakiwa mwenye miaka chini ya 18.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini