Nakala ya Rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekezwa: Ibara 28 zimefutwa, 42 Zimeongezwa….47 zimebaki kama zilivyo na 186 zimerekebishwa

 
Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba jana ilikabidhi bungeni Rasimu ya Katiba inayopendekezwa ikiwa na ibara 289 kulinganisha na 271 za Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba. 
Rasimu hiyo pia ina sura mpya mbili ambazo ni Mamlaka na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inayohusu Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Akiwasilisha rasimu hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge aliliambia Bunge kuwa Ibara 233 za rasimu hiyo zinatokana na Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Chenge, ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alisema ibara 47 za Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba zimebaki kama zilivyokuwa, 186 zimefanyiwa marekebisho, 28 zimefutwa na 41 ni mpya.
Rasimu hiyo ya Katiba inayopendekezwa imefuta kabisa muundo wa Muungano wa shirikisho ambao ungezaa muundo wa serikali tatu na badala yake imerudisha muundo wa sasa wa serikali mbili.
Chenge alisema kamati za Bunge hilo pamoja na wajumbe walio wengi, waliona kuingiza muundo wa shirikisho ilikuwa ni kukiuka makubaliano ya Muungano yaliyofikiwa mwaka 1964.
Kwa kurejesha muundo wa serikali mbili uliokuwa ukipigiwa chapuo na CCM, Rasimu hiyo imependekeza kuwapo kwa makamu watatu wa rais.
Chenge alisema uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgombea mwenza atakayekuwa makamu wa kwanza wa rais.
Chini ya muundo huo, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), atakuwa makamu wa pili wa rais ilhali Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa makamu wa tatu wa rais.
Chenge alisema mapendekezo hayo yamezingatia ukweli kuwa kuwapo kwa mgombea mwenza anayekuwa makamu wa kwanza wa rais, kutafanya rais na makamu wake kutoka chama kimoja.
Rasimu hiyo inayopendekezwa, imepunguza Tunu za Taifa kutoka saba zilizokuwamo kwenye Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba hadi nne huku mambo ya muungano yakiongezwa kutoka saba hadi 14.

Katika Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Tunu za Taifa zilikuwa ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa; sasa zimebaki Lugha ya Kiswahili, Muungano, utu na undugu na amani na utulivu. Tunu tatu ambazo ni uzalendo, uadilifu na umoja zimeondolewa.

Mambo ya Muungano

Katika Rasimu ya Tume, mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ulinzi na usalama.
Mambo mengine yalikuwa ni uraia na uhamiaji, sarafu na benki kuu, mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa, ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Rasimu inayopendekezwa imetaja mambo ya muungano kuwa ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama, usafiri wa anga, uraia, uhamiaji, polisi, sarafu na benki kuu na kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na bidhaa zinazotengenezwa Tanzania na kusimamiwa na idara ya forodha.
Mengine ni mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa, Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani, elimu ya juu, Baraza la Taifa la Mitihani, Utabiri wa Hali ya Hewa na utumishi Serikali ya Jamhuri.
Mambo mengine ambayo yalikuwa katika Rasimu ya Warioba yaliyowekwa kando ni pendekezo la wabunge kutokuwa mawaziri ikipendekezwa utaratibu wa sasa wa wabunge kuwa mawaziri uendelee kutumika.
Chenge alisema Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, imeweka ukomo wa mawaziri kuwa wasizidi 30 wakati naibu mawaziri watateuliwa kulingana na mahitaji mahsusi. Tume ya Warioba ilipendekeza mawaziri wasiozidi 15.
Rasimu hiyo inayopendekezwa imefumua muundo wa Bunge uliopendekezwa na Rasimu ya Warioba kuwa wawe 75 wa kuchaguliwa majimboni na watano kutoka kundi la watu wenye ulemavu, badala yake imesema muundo wa sasa uendelee ukiwa na wabunge 360 kwa sharti la kuwapo uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume.
Rasimu hiyo imetupilia mbali pendekezo la mtu anayetaka kugombea ubunge awe na elimu isiyopungua kidato cha nne na kurudisha kuwa ajue tu kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.
 
“Haki ya wananchi kumwajibisha mbunge kabla ya miaka mitano imeondolewa kutokana na mapendekezo ya kamati na wajumbe na watafanya hivyo baada ya miaka mitano,” alisema.
Rasimu hiyo imembana mgombea binafsi wa ubunge kwamba atakoma kuwa mbunge pale tu itakapotokea amejiunga na chama chochote cha siasa nchini.

Pendekezo la Warioba la kutaka Spika wa Bunge na Naibu wake wasitokane na wabunge wa Bunge la Jamhuri au kuwa viongozi wa juu wa vyama, nalo limewekwa kando na badala yake spika kupendekezwa achaguliwe miongoni mwa wabunge au kutoka kwa Watanzania wenye sifa ambao watajitokeza kuomba nafasi hiyo kama ilivyo sasa.
Hata hivyo, Chenge alisema wamependekeza Naibu Spika ni lazima atoke miongoni mwa wabunge.

Mgombea binafsi

Chenge alisema pamoja na kwamba mgombea huru wa nafasi ya urais ni haki ya kikatiba, lakini kamati yake imelazimika kuchukua tahadhari na kuweka masharti juu ya mgombea huyo.
Masharti hayo ni pamoja na kuweka kipengele katika Katiba kinacholitaka Bunge kutunga sheria itakayoweka masharti ya mgombea huru ikiwamo idadi ya watu watakaohitajika kumdhamini.
Pia sheria hiyo itaweka sharti la lazima linalomzuia kujiunga na chama chochote cha siasa, kuainisha vyanzo vya mapato vya kugharimia kampeni zake na kuweka wazi ilani yake ya uchaguzi.
Masuala ya kuingizwa kwa Mahakama ya Kadhi na kuruhusiwa kwa uraia wa nchi mbili ambayo yaliwagawa wajumbe wa Bunge hilo katika makundi mawili nayo hayakuingizwa katika rasimu hiyo.
Kuhusu Mahakama ya Kadhi, Chenge alisema kamati yake imezingatia mijadala ya wajumbe, taarifa za kamati za Bunge hilo na Katiba za nchi mbalimbali katika kufikia uamuzi huo.
Alisema katiba inayotungwa inahusu Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na Mahakama ya Juu hivyo masuala ya Mahakama ya Kadhi yanaweza kusimamiwa na sheria inayohusu mahakimu.
Kuhusu suala la uraia pacha, Chenge alisema waliozaliwa Tanzania lakini wakapoteza uraia na kuamua baadaye kurudi nchini, watarejeshewa uraia wao baada ya kuukana uraia wa nje. Alisema Watanzania wanaoishi nje ya nchi wakiwa na uraia wa nchi hizo, watakapokuja nchini hawatakuwa na uraia wa nchi mbili, badala yake watapewa hadhi maalumu.
Baada ya kukamilika kwa uwasilishaji huo, Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alitoa fursa kwa wajumbe wa Bunge hilo kuipitia Rasimu jioni na leo watakutana kwenye kamati zao 12 kwa lengo la kuhakiki ni kwa kiasi gani waliyoyapendekeza wakiwa ndani ya kamati na kwenye mijadala yamezingatiwa.
Kesho wajumbe wote watakutana katika Bunge zima kwa lengo la kuhakiki kwa pamoja kuhusu yale yatakayoletwa na sekretarieti kutoka kwenye kamati za Bunge hilo. Septemba 28, wajumbe hao watakutana tena kwenye kamati kwa lengo la kupewa maelekezo ya namna ya kukaa ndani ya ukumbi na pia namna watakavyopiga kura siku inayofuata.
Sitta alisema upigaji wa kura utaanza Septemba 29 hadi Oktoba 2 na baada ya hapo itajulikana kama rasimu hiyo imepitishwa kwa wingi wa kura wa theluthi mbili kwa pande zote za Muungano au la.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini