CHADEMA IRINGA WADAI POLISI NAO WANAFANYA MAANDAMANO BILA KUJIJUA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Iringa Mjini, jana
kimeshindwa kufanya maandamano ya amani kama ilivyotangazwa kwa kile
kilichoelezwa na Mwenyekiti wake, Frank Nyalusi, kuzuiliwa na jeshi la
polisi mkoani hapa.
Nyalusi ambaye
ni diwani wa Mivinjeni, alisema kuwa maandamano yanayofanyika mkoani
hapa licha ya zuio la jeshi la polisi ni ya kisasa zaidi, kwa kuwa
yanawahusu askari wenyewe kuandamana kwa kuweka ulinzi, hivyo kuandamana
wao pasipo kujua.
Alisema jeshi la polisi linaandamana nchi nzima kwa kuwakea ulinzi
pasipo kujua kuwa, hata wananchi wanaandamana kisasa kwa kuwafuata wao
kila wanapokwenda kwa lengo la kujua kama wanachama wa CHADEMA na
wafuasi wake wanaandamana.
Alisema walitoa taarifa kwa jeshi hilo siku mbili zilizopita
wakielezea nia yao ya kufanya maandamano hayo, ikiwa ni kuitikia wito
uliotangazwa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe wa kufanya
maandamano ya amani yasio na ukomo yenye lengo la kushinikiza kusitishwa
kwa Bunge la Katiba.
Alisema pamoja na jeshi hilo kuwazuia kufanya maandamano hayo, jana
hiyo hiyo waliruhusiwa kufanya mkutano wa hadhara uliofanyika katika
mtaa wenye wafanyabiashara ndogondogo (Machinga), maarufu kama Magari
Mabovu Kata ya Kitanzini.
Wakati CHADEMA wakidai kudhibitiwa kufanya maandamano hayo, Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, alisema jeshi hilo
halijapokea barua yoyote kutoka chama hicho inayoonesha wameomba kufanya
maandamano hayo.
Akitoa ufafanuzi huo kwa njia ya simu, Mungi alisema; “Nchi hii kama
zilivyo nchi nyingine inaendeshwa kwa sheria, taratibu na kanuni.”
Alisema watanzania bila kujali wanatoka kundi gani ni lazima wafanye
mambo wanayotaka kwa kuzingatia sheria, vinginevyo mkono wa sheria
utawafukuzia.