MAJAMBAZI WAUA NA KUPORA KIBAHA MKOANI PWANI
WATU wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wanatuhumiwa kumwua mtu
mwenye umri kati ya miaka 35 na 40 ambaye jina lake halikuweza
kufahamika na kumjeruhi mwingine.
Tukio hilo lilifanyika kwenye maduka
yaliyopo kwenye Stendi Kuu ya Maili Moja wilayani Kibaha, jirani na
kituo cha Polisi baada ya watu hao kufanya tukio la uhalifu.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani Pwani lipo katika
msako mkali wa watu hao waliovamia duka liitwalo Bahati, mali ya Hashim
Kisaka wakiwa na bunduki na pia walivamia ofisi ya kukata tiketi ya
mabasi yaendayo mikoani kisha kupora fedha kwenye maduka hayo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani
Pwani, Athumani Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya
saa 2 kasoro usiku Septemba 20 mwaka huu.
“Watu hao walivamia katika maeneo hayo wakiwa na silaha ambayo bado
haijafahamika na kumuua mtu huyo kwa kumpiga na risasi ya kifuani kisha
kumjeruhi mguuni mfanyabiashara wa korosho Ambwene Mwambungu wakati wa
tukio hilo ambalo lilifanyika huku umeme ukiwa umekatika na hali
iliyofanya kukawa na giza nene na watu hao kutumia mwanya huo kutekeleza
tukio hilo,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Alieleza kuwa, kwenye tukio hilo watu hao wakiwa na silaha hiyo
walivamia katika maduka hayo na kuanza kupiga risasi hewani hali
iliyowafanya watu waliokuwa katika eneo hilo kukimbia hovyo huku
wakiacha mali zao kuhofia usalama wao, kisha kupora fedha na mali ambayo
thamani yake bado haijafahamika.
“Marehemu alifikwa na mauti wakati akipelekwa Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Pwani ya Tumbi huku majeruhi wa tukio hilo bado amelazwa
akipatiwa matibabu kutokana na majeraha ya mguu aliyoyapata,” alisema
Kamanda Mwambalaswa.
Aliwataka wananchi kushirikiana kwa pamoja kutoa taarifa mara moja
watakapobaini walipo watu hao pia kutoa taarifa mara wanapohisi watu
wasioeleweka katika maeneo yao.