UGONJWA WA EBOLA NA JITIHADA ZA SERIKALI KATIKA KUPAMBANA NAO. PIX 1
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete (kulia) akisalimiana na Wauguzi waliovalia mavazi
maalumu tayari kutoa huduma kwa abiria atayekutwa na ugonjwa wa Ebola
mara atapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
jijini Dar es salaam..
Baadhi
ya Wahudumu waliovalia mavazi maalumu wa Wodi maalumu iliyotengwa kwa
ajili ya wagonjwa wa Ebola iliyoko katika eneo la Hospitali ya Temeke
jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete (wa pili toka kushoto) akiwaangalia Wahudumu waliopata mafunzo maalumu ya kumhudumia mgonjwa wa Ebola wakati alipokagua Wodi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola iliyoko katika eneo la Hospitali ya Temeke jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete (wa pili toka kushoto) akiwaangalia Wahudumu waliopata mafunzo maalumu ya kumhudumia mgonjwa wa Ebola wakati alipokagua Wodi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola iliyoko katika eneo la Hospitali ya Temeke jijini Dar es salaam.
UGONJWA WA EBOLA NA JITIHADA ZA SERIKALI KATIKA KUPAMBANA NAO.
Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.
22/09/2014.
Ebola ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya homa ya hemorajiikimaanisha ugonjwa wa kumwagika damu bila kuganda (Viral Haemorrhagic Fevers).
Kwa
mujibu wa taarifa mbalimbali, ugonjwa huu ni hatari na unasababishwa na
kirusi kiitwacho ebola kwani kirusi hicho ni moja kati ya familia ya
virusi watatu toka katika familia yafiloviridiae.
Kuna aina tano za kirusi cha ebola ambao ni bundibugyo ebolavirus(BDBV), Zaire Ebolavirus (EBOV), Reston Ebolavirus (RESTV), Sudan Ebolavirus (SUDV) na Tai Forest Ebolavirus (TAFV).
Ni
ugongwa unaoua kwa kasi na tafiti zinaonyesha kwamba katika orodha ya
watu 10 walioambukizwa na virusi vya ugonjwa huo, basi wastani kati ya
watano au tisa hufariki.
Aina
hizo tatu za virusi, yaani BDBV, EBOV na RESTV, ndiyo inayongoza kwa
kusababisha mlipuko wa ugonjwa huo Barani Afrika wakati aina nyingine za
virusi hao wanapatikana katika nchi za Asia, yaani Ufilipino na
Thailand.
Taarifa
mbalimbali zinaonyesha kuwa kwa mara ya kwanza ugonjwa huu uliripotiwa
kutokea mnamo mwaka 1976 katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
na taarifa zinaeleza kuwa hatari ya mgojwa kupoteza maisha ni asilimia
90.
Tafiti
zinaonyesha kuwa, kuwa Popo wanaopenda kula matunda wanaeneza ugonjwa
huo bila wao kuaathirika na katika jamii yetu ugonjwa huo huweza
kuambukizwa kutoka mtu mmoja mwenye maambukizi kwenda kwa mwingine baada
ya kugusana na damu au maji maji kupitia michubuko au majeraha yaliyopo
juu ya ngozi.
Pia
watu ambao wako katika hatari ya kupata ugonjwa huo ni jamii inayoishi
karibu na jamii ya wanyama ambao mara nyingi ni Nyani, Sokwe, Tumbili
pamoja na Popo.
Licha
ya watu walio na maambukizi ya ugonjwa huo kapata nafuu, lakini bado
wanaweza kuwaambukiza wengine kwa njia mbalimbali, mfano kwa njia ya
kujamiana.
Wataalam
wanaamini kuwa virusi vya ugonjwa huo huwa havienei kwa njia ya hewa
bali kwa mtu kugusana na majimaji ya mwili, kama vile matapishi, mate,
jasho, machozi, ama manii au shahawa ya mtu aliyeathirika na ugonjwa
huo.
Kwa
upande mwingine hata Madaktari na wauguzi, wanaowatunza wagonjwa wa
ebola, watu wenye uhusiano wa karibu na mtu aliyeambukizwa, watu
wanaogusa maiti ya mtu mwenye virusi hivyo wapo katika hatari ya
kuambukizwa virusi vya Ebola.
Ishara
na dalili muhimu ya ugonjwa huu ni hali ya kutokwa na damu katika
sehemu tofauti za mwili kama vile katika ufizi, pua, katika njia ya
haja, lakini kabla mgonjwa hajafikia daraja hilo, kwanza mtu huwa na
homa kali, viwango vya joto vya mwili hupanda sana, kisha anaweza kuwa
anajisikia kutapika, na hata kutapika kwenyewe, kuharisha, na pia kuwa
mnyonge huku viungo vyake vikiwa na maumivu.