Yajue maisha ya Drogba wa pori la Selous yanavyompatia kipato
KATIKA kipindi cha miaka
minne iliyopita hadi kufikia leo, watalii wanaoenda kutembelea Pori la
Akiba la Selous lililopo katika Kijiji cha Mloka kilichopo Kata ya
Mwaseni wilayani Rufiji mkoani Pwani, wanapata fursa ya kufurahia utalii
wa aina yake pindi wanapokutana na mmoja wa wanakijiji wa eneo hilo
anayejulikana kwa jina la Mwananyika lakini kwa sasa amepewa jina la
Drogba kutokana na umaarufu aliojipatia miaka ya hivi
karibuni. Inaelezwa kuwa amefanana na Drogba yule mwanasoka anayechezea
timu ya Chelsea kwa sasa.
Imeelezwa kuwa, Kijiji
hiki ni kijiji cha mwisho kabisa kabla ya kufika kwenye geti la Mtemere,
moja ya mageti ya kuingilia kwenye pori hili. Watalii kutoka ndani na
nje ya nchi (hususani raia wa kigeni) wanapofika katika kijiji hiki
hukutana na Drogba ambaye inaelezwa kuwa amepata umaarufu mkubwa kuanzia
mwaka 2011 hadi sasa.
Wenyeji wa kijiji hiki
wanasema Drogba ni mmoja wa wajasiriamali aliyewekeza nguvu na uelewa
wake wa mambo ya wanyama pori na mazingira yao kwa kutoe elimu kwa
wageni wanaungana naye katika kuelewa tabia za wanyama. Yeye haingii
kwenye hifadhi bali anazunguka nje ya pori hili kutokana na maeneo mengi
kupitika kirahisi na wanyama kupata nafasi ya kuzunguka katika moja ya
vijiji vilivyopo kijijini humo na maeneo ya jirani.
Yeye safari zake hujulikana kama bush walk na
wageni wake hupata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu
maisha ya mwanakijiji na wanyamapori. Vitu kama dawa mbalimbali za
asili, hadithi za kale huwa ni sehemu ya vitu wanavyojifunza wageni wa
‘Drogba’.
Shughuli za Mwananyika au Drogba
Watumiaji wa njia
inayoelekea katika geti hilo wanaeleza kuwa moja ya shughuli anazofanya
Drogba ni kuelekeza wageni kwenye matembezi wanaoingia kwenye pori hilo
na kujipatia kipato cha kuendeshea maisha yake pamoja na familia yake
(anatumia lugha tatu hadi sasa, Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa).
Mwenyewe hujigamba kwa kuziita true Africa walking safari na
anapokuwa kazini huwa anavaa mavazi ya asili kabisa (baadae huvaa
mavazi ya kawaida) ambayo huyatengeneza kwa magome ya miti huku akiwa
amebeba ngao, mkuki na kikapu chake cha kubebea mitishamba na vitu
vingine anavyoweza kuvipata akiwa katika eneo lake la kazi pia
anazunguka kwenye barabara zilizopo kando kando na pori hilo na wakati
mwingine hulazimika kuingia kwenye baadhi ya mapori na kuzunguka na
wageni wake nje ya hifadhi japo wapo wanyama (wakali na wapole) wapo
katika maeneo anayotembelea.
Kwa ajili ya tahadhari na usalama anapofanya safari za miguu na wageni wake siku zote huwa anaambatana na Askari wa hoteli (campsite) waliofikia wageni wake, askari anakuwa na bunduki kwa ajili ya tahadhari kwa chochote kinachoweza kutokea.
Mara zote mgeni
anayefanya utalii katika pori hili, husindikizwa na askari wa Maliasili
na wakati huo Drogba yeye anaendelea kuzunguka nje ya hifadhi bila kuwa
na woga.
Safari zake huwa na
vituo vingi ndani yake na kwenye kila kituo kuna jambo ambalo huona ni
vyema wageni wake wanastahili kulifahamu na pia endapo mnaweza kukutana
na wanyama anatumia nafasi hiyo kuwafundisha wageni mazingira ya
wanyama.
Miongoni mwa mambo
wageni wanayofaidi wanapokuwa na Drogba ni kufundishwa namna ya kutambua
nyayo za wanyama mbalimbali ambazo huwa wanakutana nazo wakiwa
safarini.
Historia yake kwa ufupi
Hadi sasa ukifika kijiji
hicho kama mtalii ukasikia watu wanamzungumzia Drogba basi kuna
uwezekano mkubwa wakawa wanamzungumzia Drogba wanayemjua wao
anayetembeza wageni wanaotoka ndani nan je ya nchi. na sio yule ambaye
watu mbalimbali wamemzoea kumsikia (anayechezea timu ya Chelsea).
Kwa hivi sasa watu wengi
wanaeleza kuwa hata jina lake kamili hawalijui kutokana na umaarufu
aliojipatia (ni mmoja kati ya watu maarufu sana kijiji hapo) na hususani
kwa wadau wa utalii ambao hupeleka wageni kwenye pori hilo kupitia
lango la Mtemere linalopakana na kijiji cha Mloka ambapo wanyama hutoka
nje na kuzunguka vijijini na maeneo ya karibu.
Hali hii inawafanya
wageni kufanya kutembelea maeneo ya nje ya pori ambazo huwaleta karibu
na wanyama wa porini, baadhi ya wanyama wanaopatikana nje ya pori hilo
ni Swala, Nyati,Tembo, Twiga na Viboko, na wanyama wengineo ambao
huonekana katika maeneo ambayo Drogba hupendelea kuzunguka akiwa na
wageni wake.
Ni nadra sana kuweza
kumsogelea Twiga mpaka muwe na usawa wa karibu mara nyingi Drogba yeye
anamkaribia bila Twiga kutimua mbio. Inaelezwa kuwa mara chache Twiga
huvumilia kwa muda kidogo na baadae kuanza kulala akiwa na Drogba.
Unapoanza kukiacha
kijiji cha Mloka na kisha kuelekea lilipo geti la kuingilia Selous
(Mtemere) utaanza kukutana na vibao vikikuonyesha zilizopo kambi kadhaa.
Kambi nyingi za Mloka zimejengwa pembezoni mwa mto Rufiji ukiwa
unaelekea Mtemere nyingi zipo upande wa Kushoto wa barabara.
CREDIT:fikrapevu