HABARI KAMILI Kuhusu Mtoto wa Rais JK Kushinda Medali Marekani!

Mtoto wa Rais Jakaya Kikwete anayesoma shule ya kimataifa ya Feza, Khalfan Jakaya Kikwete ameiwakilisha vema Tanzania katika shindano la kusaka wanafunzi wenye akili nyingi ‘Genius Olympiad’ lililofanyika Oswego, Marekani mwaka huu.

Shindano hilo huandaliwa na Idara ya Sayansi na Elimu ya Chuo Kikuu cha New York likishirikisha shule za kimataifa duniani likihusisha kazi za masuala ya sayansi, sanaa, biashara na mazingira.

Kwa mujibu wa mtandao wa www.geniusolympiad.org, mwaka huu nchi 69 zilishiriki kwa kupeleka kazi 1,171. Kazi 401 zilikidhi vigezo na kupokewa. Shule za kimataifa za Feza ziliwasilisha kazi nne na kushinda medali moja ya dhahabu na tatu za shaba.

Kazi iliyoshinda medali ya dhahabu iliitwa ‘Vcardin’ iliyoandaliwa na kuwasilishwa na Khalfan na Seif Yahya Mhata ambao wote ni wanafunzi wa shule za Feza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Khalfan alisema kazi yao imelenga kurahisisha mawasiliano ya kimataifa kwa kuwa na njia ya uhakika ya kuwasiliana.

“Mradi huu unahusu kubadilishana kadi za mawasiliano kwa njia ya mtandao. Ni muhimu sana kwa mawasiliano hasa ya wafanya biashara, lakini inahitaji uwe na simu ya kisasa yenye intaneti au kifaa kingine chenye intaneti,” alisema Khalfan aliyekuwa amefuatana na Mhata.

Kazi nyingine kutoka Feza zilizoshinda medali za shaba ni ‘The Fault of Humanity’ iliyoandaliwa na Prince Mwemezi ambaye alipiga picha ya moto ukiunguza miti eneo la Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam na kuonyesha athari za mazingira zitokanazo na uchomaji misitu.

Medali nyingine ya shaba imeletwa katika shule ya Feza na wanafunzi wawili Goodluck Komba na Sajjad El-Amin ambao walianza kazi inayoonyesha namna mkaa unavyoweza kupatikana kupitia karatasi na takataka badala ya kukata miti.

Veronica Ndomba, mhitimu wa kidato cha sita mwaka huu katika shule ya Feza Girls, aliandaa kazi ya kuzuia uchafuzi wa mazingira ya bahari kwa kuelimisha watu kuhusu kutotupa taka, mafuta na uvuvi haramu baharini na kushinda medali ya tatu ya shaba.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini