MUHIMBILI: HATUJUI PA KUMPELEKA BABU HUYU!

Na Haruni Sanchawa

Mzee Juma Hamis Juma (70) ambaye amelazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu Mei 24, mwaka huu, amekuwa akilia, akihitaji ndugu zake wafike kumchukua kwani hajui namna ya kuwapata.
Akizungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye hospitali hiyo akiwa amelazwa katika Wodi ya Mwaisela, mzee Juma alisema kuwa ni mkazi wa Unguja, Zanzibar na alitoka huko miaka mingi iliyopita na kufikia katika Mtaa wa Living Stone, Kariakoo jijini Dar.

Alisema kuwa baada ya kufika hapo, kazi aliyokuwa akiifanya ni ulinzi ambapo mwajiri wake alishafariki dunia muda mrefu.
Alieleza kwamba, hali yake ya kiafya ilibadilika mwishoni mwa Aprili mwaka huu kufuatia kusumbuliwa na kifua, ambapo alipewa msaada na wasamaria wema hadi Hospitali ya Amana jijini Dar.

Alisema alipofikishwa Amana alilazwa lakini baada ya muda mfupi alihamishiwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.

Alisema yeye ni mwenyeji wa Mkwajuni eneo la Mwembe-Kiwete, Unguja na kutaja ndugu zake wa karibu kuwa ni Pili Chande na Hamis Chande ambao wote hao hawajui yuko wapi.

Akizungumza na gazeti hili, Afisa Ustawi wa Jamii wa Wodi ya Mwaisela, Grace Julius alisema kuwa kazi kubwa ya Muhimbili kama Hospitali ya Taifa ni kupokea wagonjwa wenye ndugu na wasio nao.
“Tulimpokea mgonjwa huyu kama utaratibu unavyosema akitokea Amana, tumemshughulikia vilivyo na sasa anaendelea vizuri,” alisema afisa huyo.

Aliongeza kuwa mzee huyo alikuwa anasumbuliwa na kifua lakini pia umri nao unachangia hivyo hawaelewi watampeka wapi.
Yeyote anayemfahamu mzee huyu apige simu namba 0788 366399 ambayo ni ya afisa ustawi wa jamii.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …