MSIBA! MWANAFUNZI KIDATO CHA KWANZA AFIA BWAWANI JIJINI DAR!

Na Kulwa Mwaibale  

MSIBA! Mohamed Juma (14) ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Shule ya Sekondari ya Toangoma wilayani Temeke, Dar amefia bwawani wakati akiogelea.
Tukio hilo lililoacha majonzi kwa ndugu, jamaa, marafiki na wanafunzi wenzake, lilijiri Juni 26, mwaka huu, majira ya alasiri.

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Shule ya Sekondari ya Toangoma wilayani Temeke, Dar, Mohamed Juma (14) amefia bwawani wakati akiogelea.
 Akizungumza na Uwazi kwa masikitiko makubwa ya kumpoteza mwanaye, baba mzazi, Juma Shaha alisema familia yake imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mtoto wao wa kiume.
“Nashindwa nianzie wapi kuzungumza maana tumepata pigo kubwa sana kuondokewa na mwanangu wa kwanza katika uzao wetu wa watoto watatu wa kiume, inauma sana kwa kweli,” alisema Juma.


Juma alisema, majira ya saa 4 asubuhi ya siku ya tukio, Mohamed aliaga kwenda twisheni na baadaye saa 8 kuelekea 9 alasiri alikwenda kwa rafiki zake Kilakala, Kongowe.
“Jambo la kushangaza, hadi inafika saa 2 usiku, Mohamed hakuonekana nyumbani ndipo tulianza kumtafuta,” alisema mzazi huyo.


Baba Mohamed alisema alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Kongowe ambapo walimweleza aendelee kumtafuta.
Aliongeza kuwa, baada ya hapo alikwenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tuangoma ambaye aliungana naye kumtafuta bila mafanikio.

Juma alisema kuwa, licha ya kutoa taarifa Polisi Kongowe, alishauriwa kuripoti pia Kituo Kikuu cha Polisi Mbagala-Maturubai.

Alisema, wakati akirejea nyumbani kutoka kituoni, mkewe, Rahma Juma alimpigia simu na kumfahamisha kwamba rafiki zake Mohamed walipeleka nguo za marehemu nyumbani.

Aliendelea kusimulia kuwa, walipowahoji watoto hao, Gabriel na Musa walisema wakati wakijiandaa kuogelea kwenye bwawa hilo lililopo Toangoma, walimuona nyoka mkubwa ndipo walichukua nguo na kukimbia wakimuacha Mohamed.

Mzee huyo alisema walipokwenda Toangoma alikokutana na Mkuu wa Sekondari ya Toangoma, Nchimbi na vijana kadhaa wakaenda kwenye bwawa hilo.

Walipofika, vijana wanaoweza kuogelea walijitosa kwenye bwawa kumtafuta Mohamed ambapo walifanikiwa kumuibua akiwa amenasa kwenye matope huku ameshafariki dunia.

Mzazi huyo alisema kwamba, katika jambo la kushangaza, Mohamed hakunywa maji kama inavyokuwa kwa watu wanaokufa vifo vya ajali ya maji.
“Baada ya polisi kufika walinihoji nikawaeleza kisa cha mwanangu kufariki dunia ndipo wakauchukua mwili kwenye gari na kuupeleka nyumbani kwangu, tukafanya taratibu za mazishi na kumzika katika Makaburi ya Kimicha yaliyopo hukuhuku Kongowe,” alisema Juma kwa huzuni.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini