MWENYEKITI WA KIJIJI AZUILIWA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA
- Get link
- X
- Other Apps
Zaidi ya wahamiaji haramu 50 wanaoishi katika kijiji cha Tamau wilayani Bunda, mkoani Mara, akiwemo mwenyekiti wa kijiji hicho wamezuiwa kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Ofisa uhamiaji wa Mkoa wa Mara, Ally Dady jana amethibitisha kuzuiwa kwa watu hao wanaodaiwa kuwa ni raia wa nchi jirani Kenya. Dady alisema taratibu za kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watuhumiwa hao zinafanyika na kuongeza kuwa baadhi yao, wapo ambao walikamatwa wakiwa tayari wamekwishajiandikisha katika daftari hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliobainika kuwa ni wahamiaji haramu ni pamoja na mwenyekiti wa kijiji hicho, John Seda, ambaye anatafutwa baada ya kutoroka.
Aidha, ilielezwa kuwa wale ambao tayari walikuwa wamekwishajiandikisha katika daftari hilo, wameamriwa kurudisha vitambulisho hivyo kwa ofisa mtendaji wa kijiji na wa kata hiyo ya Kunzugu.
Ilidaiwa kuwa tayari watu hao wamepewa fomu maalumu ya kujieleza na ofisi ya uhamiaji wilayani hapa, ambapo vyanzo vya habari vinasema kuwa wahamiaji hao wamo askari polisi kutoka nchini Kenya ambao wanaishi kijijini hapo kinyume cha sheria.
Aidha, vyanzo hivyo vya habari vimedai kuwa watu hao wanaishi kijijini hapo kinyemela na kwamba mwenyekiti huyo aliyechaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita alitumia mbinu nyingi ya kupata uongozi huo ikiwa ni pamoja na kutoa rushwa.
Pia vyanzo hivyo vinasema kuishi kijijini hapo kwa wahamiaji hao kwa kipindi chote hicho ni kutokana na viongozi wa serikali kuwahalalisha watu hao kuishi hapo baada ya kupewa kitu kidogo, yaani pesa, mbuzi na ng’ombe.
Hata hivyo, Kaimu Ofisa Mtendaji Bernard Methew alipotafutwa na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, alisema kuwa hana taarifa yoyote juu ya jambo hilo na wala hakuna wahamiaji haramu kijijni hapo.
“Hizo habari umezipata wapi wewe, mbona mimi sijui….. kama ni uhamiaji nenda uwaulize huko huko” alisema Ofisa mtendaji huyo na kukata simu.
Gazeti hili lilimtafuta msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika Wilaya ya Bunda, ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Lucy Msoffe, ambaye alisema kuwa hana taarifa zozote kuhusu wahamiaji hao haramu.
Aidha, Lucy aliahidi kufuatilia zaidi suala hilo, ambapo baadaye alipiga simu na kusema kuwa ni kweli wahamiaji haramu zaidi ya hamsini wamezuiwa kujiandikisha katika daftari hilo kijijini hapo na kwamba taratibu za kisheria zinafanywa na watu wa uhamiaji.
Hivi karibuni wahamiaji haramu watatu walikamatwa wakiwa wamejiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, huku baadhi yao wakiwa wamejiandikisha zaidi ya mara moja katika vituo tofauti wilayani hapa.
Wakati huo huo, Ofisa uhamiaji huyo wa Mkoa wa Mara, alisema kuwa wahamiaji haramu wengi wako katika vijiji vya Nyaburundu, Karukekere na Tamau, katika Wilaya ya Bunda, na katika vijiji vya Bugwema na Masinono katika Wilaya ya Butiama, katika halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini.
- Get link
- X
- Other Apps