MAPYA Kuhusu KIIZA na SIMBA SC...Aapa Kuifunga YANGA SC!

Hamis Kiiza.

 Richard Bukos, Kampala
STRAIKA wa zamani wa Yanga, Hamis Kiiza, raia wa Uganda, juzi Jumamosi alitangaza rasmi kwamba amejiunga na Simba, jambo lililoshangiliwa na baadhi ya mashabiki wake.

Kiiza alitangaza hayo kwenye sherehe ya harusi ya mchezaji mwenzake, Emmanuel Okwi iliyofanyika katika Ukumbi wa Uma uliopo Lugogo nje kidogo ya Jiji la Kampala, kufuatia ndoa takatifu aliyofunga na mkewe Nakalega Florence kwenye Kanisa la Lubaga Miracle Center linaloongozwa na Mchungaji Robert Kayanja.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na wanasoka wengi wa Uganda, hasa wa timu yao ya taifa ‘The Cranes’, ulifikia muda wa wachezaji kujitambulisha majina yao na timu wanazotoka.

Wanasoka mbalimbali wanaocheza ndani na nje ya nchi, walijinasibu na timu zao huku wale ambao hawana timu kwa kipindi hiki wakijitambulisha kuwa ni wachezaji huru.

Utambulisho huo ulipofikia kwa Kiiza ambaye alikuwa mpambe wa bwanaharusi, aliamua kuweka wazi kuwa kwa sasa yeye ni mali halali ya Simba Sport Club ya Dar es Salaam, ingawa kuna mambo madogomadogo yako mbioni kumaliziwa.

Kufuatia kauli ya mchezaji huyo, Championi Jumatatu lililokuwepo ukumbini hapo, lilizungumza na mchezaji huyo na kumhoji juu ya taarifa zilizozagaa za kuwa mbioni na kujiunga na Mbeya City.

Baada ya kuulizwa swali hilo, Kiiza aliongea kwa majigambo akionesha yeye ni mchezaji mkubwa na kiwango chake siyo cha kuichezea Mbeya City huku akisisitiza kuwa yuko katika hatua za mwishoni za kuwatumikia Wanamsimbazi.

“Weweee mwandishiii… wa kucheza Mbeya City ntakuwa mimi? Sijaisha kiwango hicho kaka, wewe tulia, mimi ninachokuambia kila kitu kimeshakaa sawa kwa upande wangu na uongozi wa Simba, ngoja nikawatumikie Wanamsimbazi. 


“Na nakuhakikishia ni lazima niifunge Yanga ili niwaonyeshe Watanzania kuwa mimi ni mchezaji bora na walifanya kosa kubwa sana kuniacha,” alisema Kiiza akionekana aliyejifua vyema kutaka kuwaumbua waliomuacha.

Kiiza alicheza kwa mafanikio makubwa Yanga na kwa misimu minne iliyopita, yeye ndiye alikuwa mchezaji wa Yanga aliyeongoza kuifunga Simba.

Sasa anatua Simba na huenda akageuza kibao na kuwa mwiba mkali kwa Yanga watakapokutana.
Alipoulizwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Simba, Zacharia Hans Poppe alisema: Mimi nilikuwa nje ya nchi suala hilo la Kiiza kusajiliwa silijui, kama lipo wala msijali mtapewa taarifa.”

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini