Inasikitisha Sana: Akaa Miaka Mitatu Muhimbili Bila Matibabu Ya Aina Yoyote


Kijana Amosi Ng’arare Marale Sasi,(22) anayesumbuliwa na uvimbe usoni.

Alikuja Muhimbili ili akafanyiwe upasuaji India, alipelekwa akarudishwa bila kutibiwa, awaita ndugu zake hospitalini.

Kijana Amosi Ng’arare Marale Sasi,(22) mkazi wa Kijiji cha Kizaru, Kata ya Mryaza, wilayani Musoma Vijijni amepoteza mwelekeo wa maisha baada ya ndoto yake ya kusoma hadi chuo kikuu kuishia njiani kutokana na matatizo ya ugonjwa wa ajabu ambao unamtesa kwa kipindi cha miaka 18.

MUHIMBILI MIAKA MITATU
Kijana huyo ambaye yupo Muhimbili kwa zaidi ya miaka mitatu sasa alikuja katika hospitali hiyo kwa lengo la kupatiwa matibabu tangu mwaka 2011, hata hivyo, baada ya uchunguzi iligundulika kwamba matibabu yake ni mpaka apelekwe nchini India.

INDIA AFIKA HAKUTIBIWA
Katika mahojiano na mwandishi wa habari hii wiki iliyopita katika Jengo la Sewahaji, wodi namba 23, Amosi akionekana mwenye uso wenye huzuni alisema Oktoba 14, 2014 alipelekwa India kwa matibabu lakini baada ya kufika huko hakuna kilichofanyika.

“Nilipelekwa India katika Hospitali ya Apolo, tulikaa kule mwezi mzima na ofisa moja wa ustawi wa jamii kutoka hapa Muhimbili ambaye alinipeleka lakini cha ajabu ni kwamba ilipofika Novemba 19 mwaka jana, niliambiwa nijiandae kwa kurudi nyumbani (Tanzania) kesho yake.

“Niliuliza kwa nini nirudishwe nyumbani wakati sijatibiwa? Nikaambiwa kwamba ni uamuzi uliofikiwa na taarifa zaidi nitajulishwa hapa nyumbani.


Kijana Amosi Ng’arare Marale Sasi akiuguza uvimbe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

ARUDISHWA MUHIMBILI
“Tulipanda ndege Novemba 20 mwaka jana na kutua hapa Tanzania, nilirudishwa wodini Muhimbili. Niliambiwa nisubiri siku nyingine nitapelekwa tena huko India, nilishangaa nikaona ningoje.
“Sasa ni muda mrefu sijajulishwa chochote nimekua nikiishi hapa bila kujua hatima ya maisha yangu, na bado najiuliza kwa nini nipelekwe India halafu nirudishwe bila matibabu?”alihoji Amosi huku akitokwa machozi.

HISTORIA YA UGONJWA
“Nilizaliwa nikiwa sina tatizo la aina yoyote nikiwa na miaka minne baba akawa amefariki dunia nikabaki na mama ambaye alikua akitulea na ndugu zangu na kipato chake kinategemea kilimo cha jembe la mkono.
“Nilipofikisha umri wa miaka mine ndipo nilipoanza kupata tatizo hili kwa kutokwa na kipele kilichokuwa kinawasha. Mama alinipeleka hospitali mbalimbali kabla ya kupelekwa Bugando na hapa Muhimbili,” alisema Amosi.

Msemaji wa Hospitali ya Muhimbili hakupatika ambapo maofisa wake walisema yupo kwenye vikao vya uongozi.

Yeyote aliyeguswa na habari hii na angependa kumsaidia Amosi anaweza kuwasiliana naye kwa simu namba 0765 765747 au 0715 756384.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini