URAIS 2015: JANUARI MAKAMBA VS MWIGULU NCHEMBA NGOMA NZITO!
Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba
(41).HOMA ya Uchaguzi Mkuu 2015 inazidi kupanda. Wapo baadhi ya wagombea
wa urais ambao tayari wameshatangaza nia hadharani lakini wengine
wanaendeleza harakati zao chini kwa chini.
Miongoni mwa makada ambao tayari wameonesha nia ya kutaka kugombea ni
pamoja na vijana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (40) na Naibu
Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba (41).
Mwigulu ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi mkoani Singida, amekuwa
na mvuto wa aina yake kisiasa huku akionekana kupendwa zaidi kutokana na
kujiwekea nembo yake kwenye mavazi anayovaa kwa kujifunga skafu ya
bendera ya taifa.
Mbali na mvuto, Mwigulu tayari alishaanza mizunguko katika majimbo
mbalimbali nchini na kuanza kupiga kampeni za ‘kiaina’ ambapo ameonekana
kukubalika katika maeneo mbalimbali aliyopita ikiwemo Tanga na Morogoro
kabla ya kupigwa ‘stop’ na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Kuonesha kwamba amejipanga, Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu
wa CCM Bara, alizua gumzo zaidi alipokuwa akitumia usafiri wa helkopta
katika ziara zake ambazo zilikuwa zikitoa taswira kwamba kweli
anakubalika na wengi.
Kwa upande wake Makamba, Mbunge wa Bumbuli, alionesha nia mapema na
kuwafanya vijana wengi wampe sapoti katika harakati zake za
urais.Umaarufu wa Makamba pia unachagizwa zaidi ya umaarufu na misimamo
aliyokuwa nayo baba yake, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar na Katibu Mkuu
wa CCM, Yusuf Makamba ambaye alikuwa akifanya mambo mengi ya maendeleo
na kukemea matatizo mbalimbali nchini.
Naibu
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (40). Mbali na mvuto wa uongozi,
Makamba amezua gumzo zaidi baada ya kutoa kitabu chake ambacho
kinaelezea mikakati ya kuwania nafasi ya urais.
Mwigulu na Makamba wanazua msuguano mzito kutokana na kigezo cha
ujana ambacho kinawabeba, hali ambayo imewafanya wananchi wanaoamini
katika falsafa ya viongozi vijana kushindwa kupata jibu la moja kwa moja
juu ya nani atapendeza kupitishwa na chama.
Ukiachana na kigezo hicho, vijana hao ni wasomi. Mwigulu ana ya
Shahada ya Uzamili ya Uchumi, Shahada ya Uchumi na Cheti cha Uongozi
ambapo masomo yake amehitimu Chuo Kikuu cha Dar.
Makamba yeye ana Shahada ya Uzamili ya Diplomasia na Usuluhishi wa
Migogoro, Shahada ya Diplomasia na Usuluhishi wa Migogoro ambazo
amehitimishia katika Chuo cha George Mason, Marekani.
Wote wawili wana uzoefu mkubwa ndani ya chama. Mwigulu kabla ya kuwa
Naibu Waziri wa Fedha mwaka jana, amekitumikia chama tangu hatua ya
mkoa, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Umoja wa Vijana (UV-CCM) nafasi
ambazo anazitumikia hadi sasa.
Makamba naye vivyo hivyo, ana uzoefu wa kutosha chamani kuanzia ngazi
ya afisa wa mambo ya nje chini ya Rais Jakaya Kikwete ambaye pia
alizunguka naye nchi nzima katika kampeni zake mwaka 2005.
Swali la kwamba nani ataibuka kidedea kuwakilisha nafasi ya ugombea
kupitia chama chao ndilo ambalo linaleta utata kutokana na sifa za kila
mmoja, tusikilizie hadi Machi, mwaka huu pale atakapotangazwa rasmi.