TANESCO WAPEWA SIKU 7 WAUNGANISHE UMEME
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameitaka Bodi
mpya ya Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuliongoza shirika hilo kwa
ufanisi na kuhakikisha kuwa mteja mpya anapoomba umeme anafungiwa ndani
ya wiki moja.
Pia waziri huyo ameitaka bodi hiyo kuhakikisha kuwa shirika hilo
linajitegemea na hivyo kupunguza utegemezi wa fedha kutoka serikalini.
Akizindua bodi hiyo mwishoni mwa wiki, Profesa Muhongo alielezea
kukerwa na suala la wananchi kufungiwa umeme ndani ya siku 30 mara
wanapopeleka maombi hayo Tanesco na hivyo kuiagiza bodi hiyo
kulishughulikia suala hilo ili siku hizo zipungue.
“Bodi simamieni maombi ya kufungiwa umeme ambayo sasa yanaelezwa
kushughulikiwa ndani ya siku 30, hii lazima ibadilike, Watanzania lazima
wapewe umeme ndani ya wiki, zaidi ya hapo haikubaliki. “EWURA (Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji) waelezwe kuhusu suala hili ili kuona
namna ya kupunguza hizi siku, sababu wao wanahusika katika suala la
upangaji wa siku husika,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Akizungumzia haja ya Tanesco kujitegemea kifedha, alisema kwa kipindi
kirefu, serikali imekuwa inatoa fedha nyingi kuisaidia kutekeleza
miradi katika maeneo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Hivyo alitaka bodi hiyo kuonesha jinsi itakavyolibadilisha Shirika
ili misaada kutoka serikalini ipungue na ifike mahala shirika hilo
lijitegemee.
Kuhusu madeni ambayo Tanesco inadai kutoka kwa Taasisi za Umma,
binafsi na watu binafsi, Waziri Muhongo aliiagiza Bodi hiyo kulisimamia
suala hilo na kuja na mkakati utakaoliwezesha shirika hilo kukusanya
madeni hayo.
Alisema lengo la Serikali ni kuona shirika hilo linakusanya madeni
kutoka kwa wadeni wake wakubwa na wadogo ili Shirika hilo nalo liweze
kulipa madeni linalodaiwa na wadau wake.
Aidha, Profesa Muhongo ameiagiza bodi hiyo mpya kuhakikisha kuwa
shirika hilo linashirikiana na sekta binafsi katika miradi yake ya
uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme ili kufanikisha lengo la
serikali la kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 10,000 ifikapo mwaka
2025.
Alieleza kuwa, kulingana na sera zilizopo, uendelezaji wa sekta ya
umeme, unahitaji ushirikishwaji wa sekta binafsi kwa kuwa uwekezaji
katika sekta hiyo unahitaji kiasi kikubwa cha fedha za kigeni, kiwango
ambacho kinahitaji ushirikiano na sekta hizo.
Alisema Tanesco inapaswa kuonesha nia thabiti ya kuunga mkono juhudi
za serikali za kukamilisha majadiliano na wawekezaji na waendelezaji wa
miradi bila kuwakatisha tamaa.
Awali, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele aliieleza
bodi hiyo kwamba serikali ina imani kuwa uzoefu na weledi wa Mwenyekiti
na wajumbe wa bodi hiyo utasaidia katika kutatua changamoto
zinazoikabili sekta ya nishati ili sekta hiyo muhimu ichangie katika
kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kati.
Naibu waziri huyo aliwaasa wajumbe hao kuhakikisha kuwa taaluma
walizonazo wanazitumia katika kuliboresha shirika hilo. Naye Mwenyekiti
wa Bodi hiyo Dk Mighanda Manyahi alisema majukumu waliyokabidhiwa ya
kuisimamia Tanesco ni makubwa, lakini kwa kutumia taaluma zao
watahakikisha wanayatimiza ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa
uhakika kwa kuwa nchi ina rasilimali za kutosha zinazowezesha kutimiza
malengo hayo.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco anaongoza wajumbe
nane ambao ni Kissa Vivian Kilindu, Juma Mkobya, Dk Haji Semboja,
Shaaban Kayungilo, Dk Mutesigwa Maingu, Boniface Muhegi, Felix Kibodya
na Dk Nyamajeje Weggoro.