" NDOMBOLO YA JOSEPH KABILA, A KINSHASA!"

" Ndombolo Ya Joseph Kabila, A Kinshasa!"
Ndugu zangu,
Joseph Kabila yuko matatani. Picha za televisheni za mashirika makubwa duniani zinaonyesha machafuko Kinshasa. Ni machafuko yaliyotokana na maandamano ya wananchi kumpinga Kabila kubadili Katiba ili aendelee kutawala. Watu 40 inasemekana wamepoteza maisha.
Joseph Kabila, anaelekea kufuata mkondo wa watawala wengi wa Afrika, kuwa wakiingia madarakani, huwa wana hofu kubwa ya kuondoka madarakani. Safari hii Joseph Kabila anaonekana kuwa na wakati mgumu.


Hata kama si kwa maandamano ya mitaani, Wakongo wana namna nyingi za kuonyesha kutoridhishwa na watawala. Moja ya njia hizo ni kupitia muziki. Laurent Kabila, baba yake Joseph Kabila, naye ilimchukua muda mrefu kufahamu, kuwa staili ya muziki iliyoitwa ' Ndombolo' kimsingi ilichezwa kwa staili ya nyani asiye na uwezo wa kufanya chochote. Ilimhusu Laurent Kabila mwenyewe.
Na hata miondoko ya Ndombolo ilikuwa ni ya kejeli kwa Laurent Kabila. Rais Laurent Kabila alikuwa akitembea mguu mmoja ukionyesha kusuasua. Hatimaye, Ndombolo kama staili ya miondoko ya densi, ilipigwa marufuku!
Na Afrika changamoto kubwa ya marais walioingia madarakani wakiwa vijana sana, kama Joseph Kabila ( DRC) ,Yahya Jammeh ( Gambia) na Blaise Compaore ( Burkina Faso), ni ukweli, kuwa huwa na hofu ya kwenda kuishi maisha ya nje ya Ikulu wakiwa hata hawajafikisha miaka 50, na kwamba huwa na hofu ya mfumo mpya utakaokuja nyuma yao kuja kuwashughulikia.
Kwao, njia pekee ya kuepuka wanayoyahofia, ni kubaki madarakani, kwa udi na uvumba!
Inasikitisha.
Maggid.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini