SERIKALI YA KENYA YAKUBALI KUYARUHUSU MAGARI YA ABIRIA NA WATALII KUTOKA TANZANIA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema serikali
ya Kenya imekubali kuyaruhusu magari ya abiria na watalii kutoka Tanzania,
kuingia ndani ya Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Awali, Serikali ya Kenya iliyazuia magari hayo kuingia
uwanjani hapo huku ukiyatoza ushuru kwa yale yanayoingia, jambo ambalo
lililalamikiwa na wafanyabiashara wa Tanzania.
Marufuku hiyo ya Kenya kwa magari ya Tanzania, ilidumu
kwa zaidi ya wiki mbili, ambapo katika kusaka suluhu hiyo Nyalandu alikutana na
wafanyabiashara hao jijini Arusha kisha kukutana na kufanya mazungumzo na
Waziri wa Biashara na Utalii wa Kenya, Phyllis Kandie.
Katika mazungumzo yake na Kandie, Nyalandu alisema kwa
sasa magari ya Tanzania yataendelea kuingia uwanjani hapo wakati ufumbuzi wa
kudumu ukitafutwa.
Alisema kutakuwa na vikao vya kazi baaina ya Wizara ya
Utalii ya Kenya na wizara yake, ambapo vitaanzia ngazi ya watandaji, watalaamu,
makatibu wakuu na mawaziri.Alisema katika mikutano hiyo masuala mbalimbali
kuhusiana na biashara ya utalii yatazungumzwa baina ya nchi hizo mbili.
Hata hivyo, alisema katika vikao hivyo suala la mpaka wa
Bolongoja halitajaliwa wala kuwepo kwenye ajenda.
“Kwa sasa wafanyabiashara wetu wataingia Jomo Kenyatta
kama ilivyokuwa awali. Tumezungumza na kupanga kuwa na vikao kujadili na
kuzipatia ufumbuzi changamoto zote kuhusiana na sekta ya utalii.“Niwahakikishie tu katika vikao hivyo maslahi ya pande
zote yatazingatiwa, lakini suala la mpaka wa Bolongoja halitajadiliwa wala
kuwemo kwenye ajenda za vikao vyetu.“Wataalamu na watendaji wa wizara yangu watakutana na
wenzao jijini Arusha na maofisa wa Jumuia ya Afrika Mashariki watashiriki ili
kutafuta ufumbuzi wa kudumu,” alisema Nyalandu.
Kupatiwa ufumbuzi kwa tatizo hilo kumekuwa faraja kubwa
kwa wafanyabiashara na wadau wa utalii katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro,
ambapo walipongeza jitihada za haraka zilizofanywa na Nyalandu.Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wadau hao wa
utalii walisema Nyalandu ameonyesha utendaji kazi kwa vitendo na kwamba, hilo
linapaswa kuwa mfano kwa viongozi wengine.
Walisema waziri huyo baada ya kupata taarifa za
wafanyabiashara wa Tanzania kuzuiwa kuingiza magari Jomo Kenyatta, aliwafuata
kwenye maeneo yao na kuwasikiliza kero zinazowakabili kisha kufunga safari
kukutana na waziri Kandie jijini Nairobi.