WATU WATANO WAFARIKI DUNIA WAKIPELEKA MGONJWA WAO HOSPITALI
WATU
watano wakiwamo watatu wa familia moja wamekufa na wanne kujeruhiwa
baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei
alisema kuwa watu hao walikuwa wakimpeleka mgonjwa hospitali.
Kamanda
Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 5 mwaka huu majira ya
saa 6:30 mchana huko eneo la Fukayosi Tarafa ya Msata wilaya ya
Bagamoyo.
Alisema
kuwa ajali hiyo ilihusisha gari namba T 252 DCB aina ya Toyota Noah
lililokuwa likiendeshwa na Ramadhan Masapala (32) lililokuwa likitokea
kwenye kituo cha afya cha Miono kuelekea hospitali ya wilaya ya
Bagamoyo.
“Gari
hilo lilipasuka tairi la nyuma na kuacha njia kisha kuanguka bondeni na
kusababisha vifo hivyo na majeruhi hao,” alisema Matei.
Aidha,
aliwataja watu waliokufa ni pamoja na dereva Masapala, Mnamisima
Semhoro, Stamili Semhoro na Nemganga Semhoro wote wakazi na wakulima wa
Miono.
Aliwataja
majeruhi wa ajali hiyo ni pamoja na mjamzito aliyekuwa akipelekwa
hospitali, Shukuru Jaba (30) na muuguzi wa kituo cha afya cha Miono,
Mariamu Omary.
Kamanda
Matei alisema miili ya marehemu hao ilipelekwa hospitali ya Wilaya ya
Bagamoyo huku majeruhi wawili wakipelekwa kituo cha afya cha Miono huku
mama mjamzito akiandaliwa kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa
matibabu zaidi.