siri nzito za urais wa Jamhuri ya Muungano: Dar na Z’bar. Vikao vya Kamati Kuu ya CCM na Kamati Maalumu
Dar na Z’bar. Vikao vya Kamati Kuu ya CCM na Kamati Maalumu ya NEC
Zanzibar vinaonekana kuwa huenda vikaiweka hadharani siri nzito za urais
wa Jamhuri ya Muungano.
Mkutano wa sekretarieti ndiyo utakaoanza leo ukifuatiwa na Kamati
Maalumu ya NEC Zanzibar huku Kamati Kuu ya CCM ikitarajiwa kukutana
Jumanne wiki ijayo katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui kujadili na
kutathmini hali ya kisasa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Kikao hicho kimekuja huku wagombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho wakipishana kwa usafiri wa
ndege na boti kwenda Zanzibar kutafutwa kuungwa mkono na wajumbe wa NEC
na waliopo visiwani humo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alithibitisha kikao
hicho kufanyika Zanzibar na kitaoongozwa na Mwenyekiti wake Rais Dk
Jakaya Kikwete ambaye amebakisha muda mfupi kumaliza muhula wake wa
uongozi tangu aingie madarakani mwaka 2005.
Vuai alisema Kamati Kuu ya CCM itakutana, itatanguliwa na Kikao cha Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar.
Alisema suala kubwa ambalo watalijadili ni kuangalia mwenendo wa
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015 tangu
kumalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Hata hivyo, Vuai alisema hayuko tayari kuzungumzia ajenda ya kikao cha
Kamati Kuu kwa vile majukumu hayo yako kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi
Taifa, Nape Nnauye.
Pia, alisema Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar itakuwa na ajenda ya
mengineyo itakayojadili hali ya kisiasa tangu kumalizika uchaguzi mkuu
uliopita ambapo kikao hicho tayari matayarisho yake yamekamilika kabla
ya kuanza kamati Kuu kukutana visiwani humu.
Nape
Hata hivyo, Nape alisema jana kuwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya
CCM, inakutana leo jijini Dar es Salaam kupanga ajenda zitakazojadiliwa
kwenye mkutano wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho
itakayokutana Zanzibar Jumanne ijayo.
Alisema kuwa kikao hicho ni cha kawaida cha siku moja chini ya Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete.
Kikao cha Kamati Kuu kinakutana na kukiwa na patashika ya makada wa CCM
wanaotajwa kuwania nafasi ya urais wakipishana kwa safari za usafiri wa
majini na angani na wapambe wao kukutana na wajumbe wa NEC na mkutano
mkuu katika vikao vya faragha Pemba na Unguja kuomba ushawishi wa
kuungwa mkono.
Hali ya kisiasa Zanzibar, inadaiwa kuchafuka na kuhatarisha uimara wa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya vigogo wa Serikali hiyo
kuanza kunyosheana vidole hadharani.
Inaelezwa kuwa joto la uchaguzi wa urais ndilo ambalo limesabasisha hali
hiyo itokee. Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim, Seif Shariff Hamad na
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein huenda wakachuana katika uchaguzi
wa urais mwaka huu.
Sauala lingine zito ambalo linaweza kujadiliwa katika vikao hivyo ni la
kashfa ya escrow ambayo imewakumba mawaziri na baadhi ya madaka wa chama
hicho.
Mawaziri ambao wamekumbwa na kashfa hiyo ni pamoja na aliyekuwa Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye
ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter
Muhongo.
Profesa Tibaijuka tayari ameondolewa kwenye nafasi yake ya uwaziri baada
ya kupokea kiasi cha Sh1.6 bilioni kutoka kwa Mfanyabiashara maarufu
nchini, James Rugemarila ambaye ni mbia wa Kampuni ya Kufua Umeme ya
IPTL.
Mwingine anayetajwa kuhusika ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti,
Andrew Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba,
William Ngeleja na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo.
Mbali na wahusika wa Akaunti ya Escrow, vikao hivyo huenda vikajadili
ripoti ya maadili ya viongozi ikiwamo waliokumbwa zuio la kujihusisha na
kampeni za kuwania urais mapema kwa miezi 12, huku mienendo yao ya
kisiasa ikifuatiliwa.
Waliozuiwa kufanya kampeni ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi,
Teknolojia January Makamba, Waziri Mkuu Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven
Wassira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge
wa Sengerema, William Ngeleja.
Hata hivyo, Nape alipoulizwa kuhusiana na wagombea wa urais kufanya
kampeni za nguvu na wengine kutumia mitandao ya simu kusambaza ujumbe,
alikataa kuzungumza chochote kuhusiana na suala hilo pamoja na sakata la
escrow iwapo litapewa nafasi katika vikao hivyo vya chama.
Mtikisiko Zanzibar
Maalim Seif hivi karibuni alikaririwa akisema atapambana na Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwenye vikao vya Serikali na kulalamika
kuna baadhi ya masheha, wakuu wa wilaya na mikoa wakiwanyima wananchi
haki ya kupata vitambulisho vya Uzanzibari mkaazi na kutoandikisha
kwenye Daftari la Kudumu la Kupiga.
Akijibu dai hilo, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Balozi Seif alisema
hakuna wananchi wanaokatazwa kupata Vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi
na kueleza kuwa chini ya Sheria Namba 7 ya mwaka 2005 hakuna mtu ambaye
anaweza kupewa kama siyo mkaazi wa Zanzibar kwa miaka mitatu.
Balozi Seif alisema Serikali haitakubali kupata hasara ya kuzalisha
vitambulisho kutokana na idadi kubwa ya zaidi kuandikishwa watu ambao
siyo wakazi ya Pemba, wakati kuna vitambulisho vingi vimeshindwa
kuchukuliwa na wenyewe ambao alisema ni mamluki.
Mjumbe mmoja wa NEC ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe, alithibitisha
vigogo wanaowania urais na wapambe wao kumshawishi kuingia katika kundi
lao.
Wagombea urais
Vigogo wa urais waliofanya ziara kwa nyakati tofauti hivi karibuni
visiwani Zanzibar ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano) Stephen Wasira, Mbunge wa
Sengerema William Ngeleja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye amealikwa
kuhudhuria Maulid ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) leo yaliyoandaliwa na
Mbunge wa Mpendae na Mafanyabiasha mashuhuri, Salum Turky.
Kadhalika Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa ambaye wakati wa Sikukuu ya Krismasi ya mwaka jana alikuwa Zanzibar.
CHANZO;MWANANCHI