MAJANGA...!!! NGELEJA,CHENGE WAPELEKWA MAADILI


Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za mitaa (LAAC) za Mitaa, Kangi Lugola akizungumza wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mjumbe mwenzake, Omari Nundu.
 Licha ya Bunge kuazimia kuwa wenyeviti wa kamati zake waliotajwa kuhusika kwenye kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow wavuliwe nyadhifa zao, hali imekuwa tofauti katika vikao vya kamati hizo vilivyoanza jana baada ya baadhi yao kuongoza vikao hivyo. Jana, Kamati Kuu ya CCM imeamua viongozi hao, Andrew Chenge, William Ngeleja Na Profesa Anna Tibaijuka wafikishwe Kamati ya Maadili ya chama.
Awali, walitakiwa kuachia ngazi na kamati zao katika mabano ni Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala), Chenge (Bajeti) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini).
Kikao cha 16 na 17 cha Bunge kiliazimia kuwa kamati husika za kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa 18 wa Bunge unaoanza Januari 27, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika.
Hata hivyo, jana, Ngeleja alisema anaendelea na madaraka yake, kwa kuwa hatua iliyopo sasa ni ya uchunguzi.
“Mimi naendelea na kazi zangu kama mwenyekiti wa kamati, najua uchunguzi wa suala hili bado unaendelea, baada ya hapo ikithibitika ndipo Bunge litachukua uamuzi nami sitakuwa na budi kutekeleza,” alisema Ngeleja.
Aliongeza: “Ingawa ninajua kuna shinikizo kwa baadhi ya watu kwa sababu wanazozijua wao hawapendi kutuona katika nafasi hizi.”
Kwa upande wake, Chenge alisema: “Sikuwahi kutangaza kujiondoa katika nafasi hii ya uenyekiti. Nimeshangaa taarifa zilizotolewa katika baadhi ya vyombo vya habari.”
Alisema tuhuma zinazomkabili hazimuumizi kichwa kwa sababu hazina ukweli, “Dhamira hainiumi kwa sababu siwezi kushiriki kuiba fedha za wananchi. Mimi ni kama tumbili hata hapa nitaruka.”
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Festus Limbu alisema suala la Chenge linasubiri uamuzi utakaotolewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda. “Kamati imeamua kwa busara Chenge akae pembeni na makamu mwenyekiti aongoze vikao huku ikisubiri hatua atakazozichukua Spika (Makinda)...lakini siyo taarifa kwamba Chenge kajiuzulu, siyo kweli.”
“Unajua suala hili unaweza kusema bado ni bichi, Chenge ni mwenyekiti mteule wa Spika, lakini wenyeviti wengine wanachaguliwa na wajumbe wa kamati zao, labda Spika hajaona wa kumteua au anataka kuiachia kamati ifanye uchaguzi, hili litategemea na yeye,” alisema Limbu ambaye ni Mbunge wa Magu (CCM)
Kuhusu wafadhili wa maendeleo ambao kamati hiyo ilikutana nao jana alisema wametoa asilimia 50 ya Dola 558 milioni ambazo wahisani hao waliahidi.
Kikao cha Kamati ya Nishati na Madini kiliongozwa na Makamu mwenyekiti wake, Jerome Bwanausi ambaye alilithibitishia gazeti hili kwamba hawakufanya uchaguzi wowote.
Alipotafutwa kwa simu Mwabalaswa na kutakiwa kuzungumzia hatima yake, alijibu kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwenye simu.
Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Suala halipo kikanuni, bali ni maagizo yaliyotolewa na Bunge kwa hiyo mwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia ni Spika.”
Hata hivyo, habari zilizopatikana jana usiku ndani ya Kamati Kuu ya CCM zilieleza kuwa, Ngeleja, Chenge pamoja na Profesa Tibaijuka suala lao imeachiwa Kamati ya Maadili ya CCM chini ya mwenyekiti wake, Philip Mangula.

LAAC yalishukia jiji
Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeitaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo itoe taarifa za kueleweka kuhusu uuzaji wa hisa zake na mikataba kwa Kampuni ya Simon Group. Uamuzi huo umekuja baada ya Mkurugenzi wa jiji hilo, Wilson Kabwe na Meya, Dk Didas Masaburi kujichanganya wakati wakijibu maswali ya uuzaji wa hisa hizo kwa kampuni hiyo ambayo inamiliki Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk Mohammed alitoa maazimio hayo baada ya kuibuka mvutano kati ya wajumbe wa kamati hiyo na Dk Masaburi na Kabwe kuhusu uuzwaji wa hisa hizo ambazo ni asilimia 21.
Mvutano uliibuka baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola kueleza kuwa mmiliki wa Simons Group, Robert Kisena alitaka kununua hisa hizo, lakini jiji lilikataa.
Kwa upande wake, Kabwe alikiri kuwa walikataa zisinunuliwe kwa sababu alikuwa na shaka kama Simon Group ingeweza kulipa fedha zote kama unavyoeleza mkataba. Hisa hizo zinauzwa kwa Sh5 bilioni.
Kitendo cha wajumbe wa kamati hiyo kulichachamalia zaidi suala hilo ambalo liliwagawa katika Bunge la Bajeti kinatafsiriwa kuwa ni kutaka kulipa kisasi baada ya Dk Masaburi wakati akitoa ufafanuzi kuhusu UDA, Mei mwaka jana katika kikao cha Bajeti, kutumia lugha ya kuudhi kwa wabunge.
Pia, kamati ilihoji kwa nini Jiji la Dar es Salaam lisivunjwe na kuwa na kitengo kidogo kutokana na kutokuwa na majukumu ya moja kwa moja kwa wananchi.
Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige kwamba kuna haja ya kuvunjwa kwa jiji hilo na badala yake kubakiwe watu wachache (meya, mkurugenzi na katibu muhtasi) ambao watashungulika na masuala mtambuka.
Alisema pia kuna haja ya kuangalia upya, sheria ambayo inaipa mamlaka halmashauri ya jiji kukusanya ushuru wa maegesho ili kazi hiyo ifanywe na manispaa za jiji hilo na kisha kutoa gawiwo kwa jiji.
Katika ziara ya LAAC iliyofanya katika manispaa za jiji hilo hivi karibuni, ilipokea malalamiko ya kutopewa fedha za maegesho kutoka jiji, jambo linalozikwamisha kufanya shughuli za maendeleo. Manispaa zote tatu, Ilala, Kinondoni na Temeke zinatakiwa kugawana asilimia 75 ya mapato ya maegesho na asilimia 25 inabaki jiji.
Akijibu hoja ya ushuru, Dk Masaburi alisema madai hayo huenda yakawa na ukweli na kuwa tatizo lililopo ni mkataba uliokuwa umeingiwa na wakala, Nation Park Solution (NPS).
Awali, Mbarouk aliupa uongozi wa jiji siku 19 kuanzia leo kuhakikisha inapeleka ripoti ya tathmini ya mali kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutokana na kushindwa kuikamilisha kwa miaka mitatu tangu kutolewa kwa agizo hilo.
PAC yataka uchunguzi NBC
Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemwagiza Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru kuteua mkaguzi binafsi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa sababu za kushuka kwa mtaji wa Benki ya NBC ambayo inadaiwa Sh22.5 bilioni na Kampuni ya Absa Group Limited ya Afrika Kusini.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alitaja maeneo yaliyosababisha mtaji kushuka kuwa ni mikopo iliyotolewa kwenye sekta ya usafirishaji, utekelezaji wa sera za Benki mama ya ABCA na mfumo wa uhasibu uliotambua mapato hewa. Iwapo Serikali itashindwa kulipa deni hilo hadi Machi mwaka huu, itapoteza asilimia 30 ya hisa zake katika NBC na hivyo benki hiyo kuwa chini ya Kampuni ya Absa ambayo ina asilimia 55 ya hisa za NBC.
Awali, kampuni hiyo ilikuwa na hisa asilimia 70 za benki hiyo lakini ikauza asilimia 15 ya hisa zake kwa Shirika la Fedha la Kimataifa.
Serikali ilikopa kiasi hicho cha fedha ili kutekeleza agizo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo mwaka 2012 iliiagiza NBC kuongeza mtaji wa biashara wenye thamani ya Sh75 bilioni, baada ya ule wa awali kushuka kwa asilimia 12.
Baada ya NBC kubinafsishwa mwaka 1997, Serikali ilibaki na asilimia 30 ya hisa na Kampuni ya Absa kuchukua asilimia 70, mtaji wa NBC ulishuka kati ya mwaka 2010 hadi 2012 baada ya benki hiyo kutoa mikopo ya magari wa Sh55 bilioni.
Baada ya mtaji wa NBC kushuka kwa asilimia 12, Benki Kuu Tanzania (BoT), iliagiza wanahisa wote watatu kuongeza mtaji. Kwa kuwa Serikali haikuwa na fedha za kuongeza katika mtaji, ilikopa Sh22.5 bilioni kwa Absa na kuzitoa kama mtaji kwa makubaliano ya kurejesha deni hilo ndani ya miaka miwili. Kuhusu taasisi ya mikopo ya Pride, Msajili wa Hazina alisema baada ya ukaguzi wa CAG walibaini kuwa taasisi hiyo iliondolewa kimakosa katika orodha ya taasisi za umma.
Alisema kutokana na hali hiyo kuna hasara ambayo serikali imeipata na kusisitiza kuwa watapokea taarifa rasmi ya uchunguzi wa taasisi hiyo uliofanywa na CAG na wataiwasilisha katika vikao vya Bunge vinavyoanza Januari 27.
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Ibrahim Yamola na Beatrice Moses

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini