Majambazi Yavamia Duka la M-Pesa na Kupora Milioni 45
MAJAMBAZI watano wakiwa na silaha za moto na mapanga wamevamia duka la fedha la Mji mdogo wa Sirari na kupora Sh milioni 45 za Kitanzania na fedha za Kenya elfu 50.
Katika
hekaheka hizo majambazi hao wamejeruhi watu wawili akiwemo mwalimu wa
shule ya msingi Sirari anayeitwa Mataigwa Muhono (30) aliyepigwa risasi
mguuni na mdogo wa mwenye duka ambaye alikuwa akitoa huduma Mara Masabi
(23) ambaye amepigwa mapanga. Duka hilo mali ya Dickson Ntari (32) lipo
hatua 20 kutoka kizuizi cha kituo cha Forodha Sirari.
Aidha
majambazi hao baada ya kumaliza uvamizi katika duka la Dickson
walivamia na maduka jirani kabla ya kukimbilia nchi jirani ya Kenya.
Kaimu Kamanda wa mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya, Sweetbart Njewike
alikiri kutokea kwa tukio hilo Alhamisi jioni ya Januari 15 mwaka huu.
Alisema
kwamba majambazi hao wakiwa na makoti meusi na mmoja aliyebeba bunduki
ya vita aina ya AK 47 akiwa katika koti jekundu alipiga risasi hewani
kudhibiti watu waliokuwa wanataka kutoa msaada na ndipo alipomjeruhi
mwalimu huyo.
Pamoja
na kupora fedha taslimu Sh za kitanzania 40 ,000,000 katika duka la
Dickson pia walipora simu za mkononi 3 aina ya Samsung zenye thamani ya
Sh 850,000, simu 3 aina ya Nokia zenye thamani ya Sh 290,000.
Aidha
kwenye duka jirani linalomilikiwa na Charles Papa Nestory walipora Sh
350,000 na fedha za Kenya 50,000 wakati mfanyabiashara anayemiliki jengo
la Wazee Sirari anayetambulika kwa jina la Elisha Kaduri aliporwa
2,700,000 alizokuwa amelipwa kodi ya nyumba.
Kaimu
Kamanda huyo ACP Sweetbat Njewike alisema majambazi hao walikimbia
baada ya kuona kwamba wanaanza kuzidiwa na wafanyabiashara wengine
waliokuwa na silaha ambao walijitokeza kukabiliana nao kabla ya polisi
kufika.
Hata
hivyo alisema kwamba majambazi hao walifanikiwa kutoroka na kutokomea
porini njia ya kuelekea mji wa Isebania. Hili ni tukio la sita la
majambazi kuvamia na kupora watu fedha katika maeneo hayo ya maduka.
Katika
moja ya matukio hayo kaka mkubwa wa Dickson Ntari aitwaye Mwita Ntari
aliwahi kuvamiwa na kuporwa zaidi ya Sh milioni 60 na watu waliokuwa na
silaha za moto.
Aidha wameshawahi kuvamia baa ya ya Mzalendo mali ya Ikonde Mrimi na kuwaua wateja wawili akiwemo raia wa Kenya na fundi ujenzi.