Majambazi yateka mabasi 6 jijini Arusha....Abiria Wavuliwa nguo na kuporwa, Wanawake wanyang'anywa hadi shanga na vitu vingine vya ndani
WATU zaidi ya 40 wanaodhaniwa kuwa majambazi, wameteka mabasi sita ya abiria yanayofanya safari kati ya Jiji la Arusha na Nairobi, Kenya na kupora mali na fedha ambavyo thamani yake haijafahamika.
Tukio
hilo ambalo limethibitishwa na Jeshi la polisi, mkoani Arusha llitokea
usiku wa kuamkia jana katika eneo la Mbuga Nyeupe, wilayani Longido Mkoa
wa Arusha baada ya watu hao kuweka mawe barabarani na kuwamuru abiria
wote kutemka mmoja baada ya mwingine, kulala chini na kuwapekua kila
kitu walichokuwa nacho.
Akisimulia
mkasa huo, dereva wa basi la Perfect Trans, Joseph John, alisema kuwa
watu hao waliokuwa na silaha za jadi yakiwamo mashoka, mapanga na sime,
waliteka mabasi hayo majira ya saa 8 usiku.
“Hao
jamaa walikuwa kama 50 hivi kwani waliteka magari yetu ambayo yalikuwa
yamefuatana, wametuvua hadi viatu, saa yaani walipekua hadi wanawake
waliamriwa kuvua nguo na kuporwa urembo wenye nakshi ya madini ya vito,” alisema John.
Alisema
yeye alikuwa dereva wa kwanza kufika na basi katika eneo hilo na kuwa
alipoona mawe yamepangwa kati kati ya barabara, aliamua kusimama na
alipokuwa akijaribu kuyakwepa, alipigwa jiwe usoni hali iliyomfanya
ashindwe kukimbia.
“Hata
wengine walikuwa hawajafunika nyuso zao, tukio lilidumu kwa dakika
zaidi ya shirini, kila walipomaliza kupekua watu wa basi moja
waliwaamuru warudi ndani ya gari,” alisimulia.
Dereva
mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jabir Athumani, alisema baadhi
ya majambazi hayo yalikuwa yakiita majina ya baadhi ya watu na kuwaamuru
kutoa fedha walizokuwa nazo.
“Tunaomba vyombo ulinzi na usalama vifuatilie tukio hili kwa umakini wa hali ya juu ili kuwanasa wahusika wa tukio hili,” alisema Jabir.
Aidha,
alililitaka Jeshi la Polisi lirudishe magari ya doria katika barabara
ya Arusha–Namanga ambayo yaliondolewa Aprili mwaka jana.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kulitolea ufafanuzi leo.
“Hapa
nipo katika majukumu mengine, sipo ofisini nitawapa taarifa za tukio
lote Jumatatu (leo) mchana, naomba subiri nitafanya mkutano na vyombo
vya habari na nitawapa maelezo ya tukio lote,” alisema Sabas.