Kenge 149 wanaswa Uwanja wa Ndege Dar Wakitoroshwa nje ya nchi
Jeshi la Polisi
la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)linamshikilia
raia wa Kuwait kwa tuhuma za kukutwa na viumbe hai aina ya Kenge 149
wenye thamani ya Sh 6.3 milioni.
Kamanda wa
Polisi wa JNIA, Khamis Suleiman alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Hussain
Ahmed Ally Mansour(34), raia wa Kuwait ambaye alikamatwa uwanjani hapo
jana majira ya saa 5 usiku wakati akijiandaa na safari ya kuelekea
nchini Kuwait kupitia Dubai na Shirika la Ndege la Emirates .
Kamanda
Selemani alisema Mansour alikamatwa na wanyama hao ambao aliwahifadhi
kwenye mifuko midogo midogo ilivyowekwa katika begi kubwa lenye rangi
nyeusi.
“Kenge
waliwekwa kwenye mifuko midogo midogo 15 na kila mmoja kuna kenge 15 na
mifuko mingine walikaa wawili,”alisema kamanda Selemani.
Alisema kati ya Kenge hao, 15 walikufa na walio hai walikuwa 134 ambao walikuwa wamefichwa kwenye mifuko hiyo.
Seleman alisema
wakati wanafanyiwa upekuzi ndipo walipogundua kuna vitu ambavyo
vinafanana na nyoka na kuamua kuwashirikisha wataalamu wa maliasili
ambao walibaini kuwa begi hilo lilikuwa na Kenge.
“Huyu mtuhumiwa
alikuja nchini Januari 6,alitiliwa mashaka na polisi wa JNIA na
tulimuamuru akae pembeni kwa upekuzi zaidi na kugundua anasafirisha
kenge bila Kibali,”alisema Selemani.
Selemani
alisema walipoendelea kumuhoji mtuhumiwa huyo alidai kuwa alikuja nchini
kwa ajili ya kuchukua viumbe aina ya ndege lakini baada ya kuwakosa
aliamua kubeba Kenge hao.
Kamanda
Selemani aliwaomba wananchi kuwa na uzalendo wa nchi yao wanapoona mtu
anasafirisha rasilimali za nchi watoe taarifa katika jeshi la polisi.
Alisema polisi
wataendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo ya mipakani na viwanja vya
ndege ili kudhibiti aina hiyo ya utoroshaji wa nyara.
Julai 31, mwaka
jana raia wa Vietnam, Dong Van (47) naye alikamatwa uwanjani hapo
akiwa na meno 65 na kucha 447 za simba zenye thamani ya Sh189.4 milioni.