Hatimaye MWIGULU NCHEMBA Atoa Ufafanuzi Baada ya Kuhojiwa na TAKUKURU

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Mashariki ameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Singida kwa kumwita yeye na kumhoji kwa kuwa hilo ndilo jukumu lao la msingi.

Mwigulu aliyasema hayo wakati akitoa ufafanuzi juu ya kuhojiwa kwake na taasisi hiyo kuhusu tuhuma za kukiuka Sheria ya gharama za Uchaguzi na Sheria za Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini.

Alisema yeye kama kiongozi wa serikali hana budi kuwapongeza Takukuru kwa kutimiza wajibu wao ipasavyo, kwani kisheria taasisi hiyo ikipokea tuhuma au malalamiko yoyote, inapaswa kumhoji, kumchunguza na hatimaye kumchukulia hatua stahiki mtuhumiwa anayehusika.

Hata hivyo, alisema hajawahi kutoa rushwa ya aina yoyote tangu mchakato huo wa uchaguzi uanze jimboni Iramba na kudai kuwa anakubalika kwa wananchi.

“Hata kama nisingekwenda kufanya kampeni, nina uhakika ningepata robo tatu ya kura kwa kila kata kwa kuwa nakubalika jimboni kwangu”.

Alisema yeye ni mmoja wa watu ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kupambana na rushwa nchini; hivyo haoni sababu ya kutoa rushwa.

“Hata sababu ya kutoa rushwa sina. Nimefanya kazi yangu vizuri jimboni na kila mtu ananikubali,” alisema Mwigulu na kuongeza:

“Hiki walichofanya Takukuru ni jambo jema. Isiwe kwa Iramba tu bali pia lifanyike maeneo mengine ambako wana mashaka kuna vitendo vya rushwa. Hii ndiyo kazi ya serikali katika kuhakikisha wale wote wanaokiuka kanuni na taratibu za uchaguzi wanashughulikiwa ipasavyo.”

Alisema kuwa katika uchaguzi wowote ni lazima kuwepo na changamoto mbalimbali, lakini kwa masuala anayolalamikiwa na wagombea wenzake, kimsingi walishakubaliana kwenye vikao vya kamati ya siasa ya chama hata kabla ya kuanza mchakato; hivyo yeye anashangaa wenzake walivyomgeuka.

“Kwa mfano, tulikubaliana tuwe na gari moja kila mgombea kwa ajili ya matangazo, mimi la kwangu ni Fuso wao wanatumia Canter na zina spika. Sasa kama spika zangu zimezidi nguvu za kwao hiyo siyo hoja… ni mambo tuliyokubaliana wenyewe tuendelee na mchakato,” alisema na kuongeza kwa lugha ya utani:

"Wasilete mambo ya mpira wa kizamani ambapo timu isiyo na viatu hugomea mchezo hadi wenzao nao wavue viatu ndipo wacheze (yaani: ‘hatuchezi mpaka na ninyi mvue viatu’)”.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini