Mbaroni kwa kuoa binti wa darasa la 6

JESHI la Polisi wilayani Nkasi katika mkoa wa Rukwa linamshikilia kijana mmoja, Nkuli Lenganija (22) kwa tuhuma ya kuishi kinyumba na mwanafunzi wa kike kwa miezi miwili.

Pia, linawasaka wazazi wanaodaiwa kumwozesha binti yao huyo mwenye umri wa miaka 14, ambapo tayari wamepokea mahari ya ng’ombe 15.
Msichana huyo ni mwanafunzi wa shule ya msingi Katani na anasoma darasa la sita.
Inadaiwa kuwa wazazi wa Nkuli walitoa mahari hiyo kwa wazazi wa msichana ambaye alilazimishwa kukatiza masomo yake na kuishi kama mke na kijana wao kwa zaidi ya miezi miwili sasa.
Tayari Jeshi la Polisi wilayani hapa, linamshikilia kijana huyo akituhumiwa kuishi kinyumba na mwanafunzi huyo wa kike kwa miezi miwili sasa huku likiwasaka wazazi wake kwa tuhuma za kumwozesha kijana wao mtoto wa shule.
Akielezea mkasa huo mjini Namanyere wilayani hapa juzi, Mkuu wa Dawati la Wanawake, Jinsia na Watoto wa Wilaya ya Nkasi, Anna Kisimba alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa jana saa 4: asubuhi kijijini Chonga akichunga ng’ombe za wazazi wake.
Akifafanua, Kisimba alidai kuwa miezi miwili iliyopita wazazi wa msichana na mvulana huyo walikutana na kukubaliana kuwa watoto wao waoane.
“Ndipo wazazi wa mvulana walipolipa mahari ya ng’ombe 15 kwa wazazi wa msichana kisha wakamkabidhi kijana wao msichana huyo kwamba ni mke wake,” alieleza Kisimba.
Mtuhumiwa Nkuli anadaiwa kuishi kijiji cha Chongo, akichunga idadi kubwa ya ngombe wa wazazi wake, ambao wanaishi katika kijiji kingine cha Katani na wazazi wa msichana.
Ilidaiwa miezi miwili iliyopita baada ya kulipa mahari hiyo, wazazi wa msichana walimkabidhi binti yao huyo, ambapo “wakwe” zake walimchukua na kwenda naye malishoni na kumkabidhi kijana wao .
Mtuhumiwa huyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa hajawahi kuingia darasani wala hajui kusoma na kuandika .
“Maisha yangu yote tangu nikiwa mdogo nimekuwa nikichunga ng’ombe wa baba yangu ...waliponiletea msichana huyo nilimpokea na kuishi nae kama mke,” alieleza.
Msichana huyo alidai kuwa yupo tayari kurudi shuleni kuendelea na masomo na kwamba alilazimishwa kuolewa huku umri wake ukiwa bado mdogo .
Taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi wilayani hapa, zilidai kuwa bado wanaendelea na msako wa watuhumiwa hao wengine ili sheria ichukue mkondo wake.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini