HUJAFA HUJAUMBIKA! MKASA WA MWANAFUNZI HUYU UNASIKITISHA SANA...SOMA HII TAFADHALI
“Natamani nirudi shuleni hata kama ni darasa la kwanza, kama siyo ugonjwa huu wa ajabu ningekuwa namaliza kidato cha nne mwaka huu,” ni maneno ya kijana Frank Ephraim Simon (17), mkazi wa Kijiji cha Viwege, Gongo la Mboto jijini Dar akizungumza na Amani juu ya mateso anayopata.
…Akinyanyuliwa kutoka kwenye kiti.
Kwa mujibu wa dada wa Frank aliyejitambulisha kwa jina la Adela Ephraim aliyekutwa akimhudumia na ndugu zake kijijini hapo, tatizo la ndugu yake huyo lilianza mwaka 2008 akiwa mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi ya Toangoma, kabla ya kuhamia Viwege.
Akiwa ameketi.
“Alianza kwa kuishiwa nguvu mwili mzima na kuanguka kila alikokwenda. Tatizo hilo lilidumu kwa miezi kadhaa kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya CCBRT, Dar.
“Hata hivyo, tatizo halikuonekana zaidi ya kushauriwa awe anapelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya mazoezi ya viungo.
“Hali yake ilizidi kuwa mbaya kila kulipokucha, akawa anaanguka mara kwa mara, ikabidi asiendelee na masomo kwa muda ili atibiwe gonjwa hilo la ajabu.
“Kuna kipindi alikuwa kama amepona, akawa haanguki tena lakini baadaye hali ilibadilika na kurudi kama awali.
“Kufariki kwa baba yetu mwaka 2011, kulichangia kudhoofika kwa mdogo wetu, hasa baada ya mama wa kambo kuziteka mali zote, tukakosa hata nauli ya kumpeleka hospitalini.
“Kama unavyomuona (akimuonesha mwandishi) hawezi kutembea, kujigeuza, amekuwa ni mtu wa kulala, kila kitu ni wa kusaidiwa, akishika kitu mikono inatetemeka, akilala sehemu moja kumgeuza ni shida kwa sababu ni mzito mno kwani kichwa pekee ndiyo kizima, sehemu zingine za mwili ni kama amepooza.
“Tunaomba Watanzania, taasisi au kampuni itakayoguswa na tatizo hili watusaidie ili tuendelee kumtibu ndugu yetu kwani hatujui nini hatima yake,” alisema dada huyo.
Kwa upande wake denti huyo alisema: “Watanzania, ninaomba msaada wenu, Rais Jakaya Kikwete na viongozi mnaosoma Gazeti la Amani, ninaomba msaada wenu.
Kwa yeyote aliyeguswa kumsaidia kijana Frank ili akapatiwe matibabu kama mwanzoni, awasiliane na dada yake kupitia simu ya mkononi namba 0659406588.