Tundu Lissu Azungumzia Wanaotaka Kuihama CHADEMA Baada ya Lowassa Kupokelewa na Chama Hicho!
Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA Tundu Lissu, amesema chama chao kinatarajia kupata wanachama wengi baada Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kujiunga na chama hicho.
Lissu ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo taarifa kwamba wapo wanachama wa CHADEMA ambao watakihama chama hicho kutokana na kutokubaliana na ujio wa Lowassa ndani ya CHADEMA.
Akizungumza jana na waandishi wa habari Lissu alisema,
“Kama wapo watakao jiondoa CHADEMA, wengi zaidi watakuja. Tupo katika kipindi ambacho hatujawahi kuwepo tangu mfumo wa vyama vingi uanze. Mfumo tawala unabomoka vipande vipande. Unapobomoka, dalili zake ni watu ambao wamekuwa katika mfumo huo kuondoka kama alivyofanya Lowassa.”
“Mabadiliko katika nchi yanatokea pale mfumo tawala unapo pasuka. Lowassa ni mfano mzuri.
"Tunamkaribisha kwetu siyo kwa sababu ni mwanasiasa msafi. Tumempokea kwa sababu tunaongeza nguvu kubwa kwa wale wanaotaka mabadiliko. Imetokea Zambia Mawawi, Nigeria na Kenya”
Akizungumza kuhusu CHADEMA kumtuhumu Lowassa kwamba “ni fisadi” kabla ya kujiunga na chama hicho Lissu alisema;
“…hatukuwa na makosa hata kido kumweka Lowassa katika kundi la watuhumiwa wa Richmond. Mambo yalizungumzwa bungeni. Aliwajibika na amesema mwenyewe aliwajibika.”
“Alijiuzulu Uwaziri Mkuu kwa sababu ya Richmond. Tulimweka katika orodha ya mafisadi kwa sababu ya Richmond. Na jana alisema alimwambia rais “tuvunje mkataba” rais akaataa. Angefanyeje? Hilo ni vumbi, litakapotulia Chama Cha Mapinduzi na mfumo tawala utakuwa umeanguka, tutajenga nchini. Bila kuvunja mfumo tawala hakuna kusonga mbele,”