MADAI MAZITO: FLORA MBASHA Amshtaki Tena Mumewe!
Mwimba Injili Flora Mbasha na mwandani wake wa zamani, Emmanuel Mbasha.
Brighton Masalu
WAKATI aliyekuwa mumewe akiwa na msala wa kubaka shemejiye mahakamani, mwimba Injili Flora Mbasha amemshtaki tena mwandani wake huyo wa zamani, Emmanuel Mbasha akidai kumpa vitisho mara kwa mara.
Emmanuel Mbasha.
Chanzo kilicho karibu na Flora kilipenyeza habari kuwa mara kwa mara Mbasha amekuwa akimtishia Flora ndipo mwanamuziki huyo alipoamua kumshtaki polisi.“Jamaa (Mbasha) alikuwa akitumia watu kumtishatisha Flora sasa Flora akaamua kwenda kumshtaki polisi Msimbazi maana ameona lolote linaweza kutokea hivyo awe tayari ameshatoa mashtaka polisi,” kilisema chanzo hicho.
Mwanahabari wetu alipomtafuta Flora na kumuuliza kama amemshtaki Mbasha, alikiri na kubainisha kuwa alifanya hivyo kutokana na vitisho mbalimbali alivyokuwa anavipata.
“Ni kweli ilibidi niende pale Msimbazi Polisi, nikapewa jalada uchunguzi MS/RB/7000/2014. Mbasha amekuwa akinitishiatishia sana, mara aniambie nitahama nchi niende nikaishi kwa ndugu zangu Marekani,” alisema Flora.
Alipotafutwa Mbasha na kusomewa mashtaka yake, alisema Flora ni muongo na anatafuta kujitetea mbele ya jamii aonekane ni mwema.
“Hana lolote huyo muongo tu, nilisikia hata mimi kuwa amenishtaki lakini nafikiri hata polisi hawakulipa uzito jambo hilo na yaliisha hivyohivyo,” alisema Mbasha.
Mbali na tukio hilo, Mbasha anakabiliwa na kesi ya kumbaka shemeji yake kosa analodaiwa kulitenda mwaka jana, jijini Dar. Juzi Alhamisi alifika katika Mahakama ya Ilala na kutoa utetezi kisha kesi ikaahirishwa hadi Agosti 14, mwaka huu.