Sheria mpya ya wafungwa watakaogoma kula chakula Gerezani
Bunge la Israeli, limepitisha sheria ya kuwalisha kwa lazima wafungwa ambao wanashiriki mgomo na kususia kula.
Sheria hiyo ambayo ilikubaliwa na idadi kubwa ya wabunge, inawaruhusu mahakimu kuhakikisha kuwa wafungwa wanalishwa kwa lazima na pia kupata matibabu kwa lazima bila ya ruhusa ya mfungwa ili kunusuru maisha yao.
Raia wa Palestina ambao wanazuiliwa katika magereza ya Israeli wamekuwa wakisusia chakula kama njia yao ya kupinga kukamatwa kwao katika miaka michache iliyopita.
Nchi hiyo inahofu kuwa wafungwa hao ambao wamekataa kula chakula huenda wakafa na kusababisha fujo magerezani.
Sheria hiyo mpya imelaaniwa na chama cha madaktari nchini Israeli, ambacho kinaamini kuwa kuwalisha wafungwa chakula kwa nguvu ni mbinu ya mateso na ni hatari kimatibabu.